Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi Kimara walazimisha basi la Udart kupakia abiria

46608 U+dart+pic

Thu, 14 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakazi wa Kimara Mwisho jijini Dar es Salaam jana walichukua hatua ambayo inaweza kuwafanya waendeshaji wa mradi wa mwendokasi kufikiria upya utaratibu wao.

Huku mabasi ya kampuni ya Udart inayoendesha mradi huo yakiwa yamepungua, usafiri umezidi kuwa mgumu katika maeneo yanayohudumiwa na mradi huo.

Kwa mujibu wa utaratibu wao, baadhi ya mabasi ya mradi huo hayaegeshwi eneo la ofisi zao zilizopo Jangwani. Na hata kama liliegeshwa Kimara, alfajiri hulazimika kuondoka bila abiria kutoka kituo hicho na kwenda kupakia abiria katika kituo cha ruti lilikopangiwa.

Lakini wakazi wa Kimara walionekana kuchoshwa na utaratibu huo na hawakuwa tayari kuona mabasi hayo yakiondoka bila abiria hata mmoja.

Na katika kuonyesha kutokubaliana na hali hiyo, jana asubuhi umati wa watu waliokuwa kituo cha Kimara wakisubiri mabasi hayo, waliamua kuingia katika barabara maalumu za mabasi hayo na kuzuia basi moja lililokuwa linataka kwenda bila abiria na kufanikiwa kulazimisha kubeba abiria.

Wakizungumza na Mwananchi jana katika kituo cha mabasi hayo abiria hao walilalamikia utaratibu huo wa Udart na kuiomba Serikali kuingilia kati kurejesha ubora wa huduma hiyo.

Pia abiria hao wameiomba Udart kuongeza mabasi au kufuta safari hiyo kwa kuwa usafiri umekuwa mgumu.

Walisema mabasi mengi hufika kituoni yakiwa yamejaa jambo linalosababisha wengi wao kuchelewa makazini na wanaoweza kupanda ni wenye mabavu kutokana na fujo.

Mmoja wa abiria hao, Boniface Liuchi alisema kama mabasi hayo yamepungua, Udart wafute ruti ya mabasi yanayotoka Mbezi kuja Kimara kauli iliyoungwa mkono na abiria wengi waliokuwepo eneo hilo.

“Miezi kadhaa iliyopita, mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, (Paul Makonda) alitembelea kituo cha Kimara, taabu zilipungua. Lakini wiki tatu baadaye mambo yamejirudia,” alisema Ramadhani Ali akimuunga mkono Liuchi.

Jitihada za kuwapata Udart na Dart kuzungumzia hali hiyo hazikuzaa matunda. Wakati mabasi yakiwa machache, kuna mabasi 70 yanayoshikiliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo Jumamosi ya Machi 16, yatafikisha mwaka tangu kushikiliwa kwake, mamlaka hiyo bado imesisitiza ili kuwachiwa lazima yalipiwe kodi.

Mabasi hayo 70 yaliingizwa nchini tangu Februari 16 mwaka jana na Udart kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo akizungumza na Mwananchi alisema bado wanayashikilia mpaka sasa kutokana na wahusika bado hawajakamilisha taratibu za kuyalipia kodi.



Chanzo: mwananchi.co.tz