Wakazi wa Kijiji cha Idunda, Kata ya Kimala, mkoani Iringa wamemwomba Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga asaidie ujenzi wa daraja linalohatarisha maisha yao hasa kwa watoto.
Wamesema tatizo hilo si kwa sababu ya mvua, badili ni la miaka mingi, eneo hilo halina daraja jambo lililokifanya kijiji chao kuwa kama kisiwa.
Wamesema hayo wakati wa ziara ya mbunge huyo inayolenga kuangalia maeneo yasiyopitika ili yarekebishwe.
"Kila siku wanafunzi wa Sekondari wanavuka hapa kwenda na kurudi kutoka shule, daraja halipitiki, wajawazito wanapita hapahapa na matumbo yao, ukivuka maji yanafika juu ya kiuno, tunaomba msaada," amesema Ester Ndali, mkazi wa eneo hilo.
Kastory Msingu (81), mkazi wa Idunda amesema licha na umri wake mkubwa, naye hulazimika kuvuka kwenye eneo hilo, jambo ambalo ni hatari.
"Nikitoka kwenda kutibiwa lazima nivuke kwenye haya maji, wakati mwingine yanakushinda nguvu lakini utafanyaje? Niombe watutengenezee daraja," amesema Msungu.
Kutokana na hali hiyo, Nyamoga aliiwataka Wakala wa Barabara Vijini (Tarura) kutenga fedha za dharura kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili.
"Tusingoje mpaka mtu azame, apoteze maisha ndio tuje kutengeneza daraja hili, tutengeneze mapema kwa sababu kilio hiki ni cha muda mrefu," amesema Nyamoga. Mhandisi wa Tarura Wilaya ya Kilolo, Edward Chacha amesema changamoto hiyo wataifanyia kazi ili daraja liweze kujengwa.