Dar es salaam. Wakazi wa Kata ya Tabata na Bonyokwa jijini Dar es Salaam wamemueleza Waziri wa Maji ya Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa kuhusu kero ya maji katika maeneo yao, huku waziri huyo akikiri udhaifu wa watendaji katika kushughulikia kero hizo.
Profesa Mbarawa amesema huduma za maji ni sehemu ya ahadi muhimu iliyopewa kipaumbele katika Ilani ya CCM, lakini wananchi wa mikoa hiyo bado wanalalamikia upatikanaji wa huduma hiyo.
Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Desemba 4, 2018 katika ziara yake ya kukagua huduma za maji katika jiji la Dar es Salaam, lengo likiwa ni kushughulikia maeneo yenye kero sugu za maji.
Ziara hiyo alianza jana na leo ametembelea kata hizo mbili.
Jafarani Mwambe, mkazi wa mtaa wa Kilimani Kata ya Bonyokwa amesema wakazi wa mtaa huo wamekuwa wakitumia maji ya visima vya ujenzi.
"Kila siku alfajiri tunaenda kuvizia kuiba maji kwenye majengo ya watu, matokeo yake kila ukipima magonjwa tunayopata ni kichocho, zaidi ya miaka kumi iliyopita tumekuwa na kilio hiki lakini ni ahadi tu kila mwaka, "amesema Jafarani.
Mariamu Mwaibura amesema kila mwezi amekuwa akitumia wastani wa Sh70,000 kununua lita 6,000 za maji yanayouzwa katika magari.
Meneja wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) katika mkoa wa kihuduma wa Tabata na Bonyokwa, Victoria Masele amesema wastani wa asilimia 75 ya wakazi wa Tabata ndio wanapata maji na kwamba Bonyokwa hakuna maji kutokana na kukosa chanzo cha kusambaza maji.
Waziri Mbarawa amewahakikishia wakazi hao kuwa kuanzia Jumatatu wataunganisha huduma ya maji Bonyokwa pamoja na kushughulika kero zinazoendelea kujitokeza.
"Bonyokwa hakukuwa na chanzo cha maji kwa hiyo kimepatikana eneo la Kimara na mabomba yameshanunuliwa,"amesema.