Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi Dar, Moro wahimizwa kutembelea vivutio Kisarawe

94a84f27efcfd7480902a8c7e282eb1f Wakazi Dar, Moro wahimizwa kutembelea vivutio Kisarawe

Sun, 7 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKALA wa Misitu Tanzania (TFS) umewaomba wananchi hususani wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na mingine ya jirani, kutembelea vivutio vya utalii vilivyoko wilayani Kisarawe mkoani Pwani ikiwamo Msitu wa Kazimzumbwi wenye vivutio vya kipekee.

Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Kisarawe, Fredy Ndandika alisema hayo katika banda la taasisi hiyo, inayoshiriki Tamasha la Kisarawe Ushoroba Festival wilayani Kisarawe mkoa wa Pwani, juzi.

Alisema moja ya maeneo yanayostahili kutembelewa na wanachi na wakafurahia ni Msitu wa Kazimzumbwi.

“Msitu huu wa asili wa Kazimzumbwi unapatikana Kisarawe na una vivutio vingi ikiwamo hali ya utulivu ambayo humpendeza kila mmoja anayeutembelea,” alisema Ndandika.

Mbali na utulivu, ndani ya msitu huo kuna njia za watembea kwa miguu, mapango ya popo na mapango ya mizimu ambayo jamii ya Wazaramo huyatumia kwa ajili ya matambiko na kuomba.

Ndandika alisema kivutio kingine kinachopatikana katika wilaya ya Kisarawe na ambacho anashauri wananchi wajitokeze kutemblea ni Bwawa la Minaki, ambalo hutumika kwa ajili ya utalii wa uvuvi na kupiga picha.

Vivutio vingine ni maeneo ya kupumzikia yenye sifa ya kuwa na hewa safi na pia maeneo ambayo yanamwezesha mtu kusimama na kuona kwa uzuri mandhari ya jiji la Dar es saalam.

Alisema Msitu wa Kazimzumbwi ndio pekee unaotegemewa kwa kunyonya hewa chafu inayozalishwa Dar es Salaam na maeneo ya jirani na Kisarawe.

“Tupo kwenye tamasha la utalii la Kisarawe Ushoroba Festival ambapo lengo kuu la tamasha hili ni kutangaza utalii na vivutio vya utalii vilivyopo ndani ya wilaya ya Kisarawe na kuonyesha fursa za uwekezaji katika wilaya yetu.

"Katika wilaya ya Kisarawe kuna utalii wa aina mbili, utalii wa kiutamaduni na utalii wa kiikolojia. Huu wa Ikolojia unapatikana katika Hifadhi ya Mwalimu Nyerere ambayo sifa yake ya pekee ni kuwa hifadhi kubwa zaidi nchini," aliongeza Ndandika

Alisema TFS ndiyo iliyopewa jukumu la kusimamia Hfadhi ya Mwalimu Nyerere na watatumia vyema siku tatu za Tamasha la Kisarawe Ushoroba, kutangaza fursa zilizopo ili kuvutia watalii na wawekezaji.

Awali akizungumza katika ufunguzi wa tamasha hilo, Mkuu wa Walaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo alisema wameamua kuchochea juhudi za kutangaza utalii wilayani mwake ili kutengeneza fursa za ajira na kuwezesha wananchi wengi, kuona vivutio mbalimbali viliyoko Kisarawe.

Jokate aliwapongeza TFS kwa kushiriki tangu mwanzo wa majadiliano kuhusu kufanikisha tamasha hilo. Alisema anawatambua TFS kuwa ni wadau wakubwa pamoja na wadau wengine.

Chanzo: www.habarileo.co.tz