Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi Bonde la Msimbazi kusaini mikataba ya fidia wiki ijayo

Bonde Mto Msimbazi.jpeg Wakazi Bonde la Msimbazi kusaini mikataba ya fidia wiki ijayo

Sat, 14 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dar es Salaam. Hatimaye watakao athiriwa na mradi wa uendelezaji wa bonde la Msimbazi, kuanza kusaini mikataba ya malipo ya fidia, sambamba na kuhakikiwa taarifa zao za kibenki, kabla ya malipo kufanyika.

Shughuli hiyo itaenda sambamba na wale ambao hawakuridhika na uthamini kuthaminiwa upya kwa kuzingatia aina ya malalamiko yao.

Mradi huo wa ambao unalenga kuzuia mafuriko, utahusisha ujenzi wa daraja la juu katika Barabara ya Morogoro, pamoja na ujenzi wa kingo mto ambapo inakadiriwa kugharimu zaidi ya Sh598 milioni.

Habari njema hiyo kwa wakazi hao, imetolewa leo Jumamosi Oktoba 14, 2023 kwa tangazo kutoka ofisi ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-Tamisemi).

Tamisemi inatekeleza mradi wa uendelezaji wa Bonde la Msimbazi kwa lengo la kukabiliana na mafuriko na kuboresha matumizi ya ardhi katika eneo la chini la bonde, ambapo inaelezwa kukamilika kwa mradi huo, kutaiwezesha Serikali kuingiza zaidi ya Sh2 trilioni.

Hata hivyo, ili kufanikisha utekelezaji wa mradi huo, Serikali inatarajia kuwahamisha watu wote watakao athiriwa na mradi, huku ikiwalipa fidia ya mali zao ambazo kimsingi zinaathiriwa na uwepo wa mradi huo.

Katika tangazo hilo, imeelezwa kuwa shughuli za ulipaji fidia, zinatarajiwa kuanza wiki ijayo Oktoba 20 na kwamba zitafanywa na Kampuni ya Property Matrix Limited kwa niaba ya Tamisemi.

Taarifa hiyo imeorodhesha ratiba ya zoezi hilo ambalo litaanza Oktoba 18, na kwamba linatarajiwa kukamilika Oktoba 30, 2023.

Hivyo basi, wote wanaohusika wametakiwa kwenda katika maeneo ya usainishwaji wakiwa na vitambulisho vya uraia (Nida) au vile vya Mpiga Kura, pamoja na nyaraka zote zinazowathibitisha iwapo wanapokea malipo kwa niaba.

Kwa wale ambao hawakuafiki viwango vya fidia walivyoonyeshwa, watafanyiwa uhakiki upya ambapo imeleezwa kuwepo kwa timu mbili za wathamini kwa Wilaya za Kinondoni na Ilala ambazo zitapita kwenye makazi ya waathirika kwa kufuata ratiba na kwamba zoezi litaanza Oktoba 19 – 24, 2023.

Taarifa imewataka wataohakikiwa upya kutoa ushirikiano kwa kuwepo katika ofisi za Serikali za Mitaa kuanzia saa 2:00 asubuhi.

Wakizungumzia hatua hiyo, Katibu, Kamati ya Wananchi, Msimbazi Bondeni Thomas Moshi, amesema wanashukuru kufikiwa kwa hatua hiyo, japo wanahoji juu ya kitakacholipwa wakisema hawakijui ikizingatiwa kuna ahadi ya kupewa viwanja Kigamboni.

“Hakuna anayepinga huu mradi kufanyika, isipokuwa suala la ulipaji fidia ndio limetawaliwa na usiri, hakuna anayejua anenda kulipwa nini, ngoja tuone wakianza kutusainisha lakini kwa ambaye hatakuwa ameridhika na atakacholipwa halazimishwi kusaini,” amesema Katibu huyo, na kujulisha kuwa watakuwa na kikao chao kesho.

Kwa upande wake Katibu Kamati ya Wananchi wa Mitaa 16 iliyo kwenye mradi, Luqman Waziri, amesema malalamiko yao makubwa ni kutolipwa ardhi huku fidia walizopigiwa za nyumba zikiwa ni ndogo licha ya kuwa na hati na leseni za makazi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live