Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi 3,700 Siha watakiwa kubomoa nyumba zao

28635 Wakazi+pic TanzaniaWeb

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Wakati Serikali ikishughulikia mgogoro kati ya wakazi 3,700 wa Kijiji cha Mlangoni wilayani Siha na Shirika la Watawa la Holy Spirit Sisters, wananchi hao wamepewa siku 14 kubomoa nyumba zao.

Agizo hilo lililotolewa na kampuni ya Udalali ya Independent Agencies & Court Broker Ltd, limekuja siku chache tu baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kutembelea eneo hilo.

Waziri Lukuvi alifanya mkutano na wananchi hao Oktoba 26 na kuwaeleza bayana kuwa kwa sasa eneo hilo ni mali ya shirika hilo la masisita na ndio walioshinda kesi Mahakama ya Rufaa.

“Mahakama ya Rufaa imeshaagiza kuwa hamna chenu na mtahamishwa pale bila fidia yoyote. Hukumu hiyo wamepewa na hamna mali yenu pale kabisa. Hamna haki hata moja,” alisema Waziri Lukuvi siku hiyo.

“Sasa mkiendelea kujenga leo, mnaweza kuwa mnapoteza nguvu ya bure maana unajengaje mahali pasipo kwako. Ndio maana nimesema ujenzi wote na shughuli zozote za maendeleo zisimame.

“Ili tuchukue data tujue waliopo leo tunapoanza kuzungumza ni akina nani na shughuli zenu. Watakapokuja kuchukua data kila mmoja aseme vizuri kwamba nyumba yangu ni hii nimekaa hapa miaka fulani.”

“Hii itatupa sababu sisi ya ushahidi wa kujenga hoja ya kutaka kuwabakiza pale. Hatuwezi kuwabakiza pale kwa sababu hivi sasa hatujui. Nyinyi mnatuambia mko 3,700 lakini kuna wanaosema hata 1,000 hamfiki.”

Aliwataka wananchi hao kuiruhusu Serikali kuchukua taarifa zao ili iweze kuwaombea wabaki eneo hilo.

“Sisi tusingependa nyumba hizo za wakazi 3,700 zivunjwe. Interest ya Serikali si kuvunja nyumba za watu. Rais ameshasema hapendi majumba ya watu yavunjwe na kuwatia hasara watu,” alisema.

Lakini wakati mchakato huo ukiendelea, kampuni hiyo ya udalali imetoa tangazo la kuwaamuru Januari Kamili Shayo na wenzake 136, waliofungua kesi kubomoa nyumba zao.

“Nimeagizwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi ninawaamuru kubomoa nyumba zenu zilizojengwa eneo ambalo si mali yenu na kuhama mara moja,” inasema taarifa hiyo iliyotiwa saini na Newton Makwale ambaye ni dalali wa mahakama.

“Kumbuka kwamba nimepewa hati ya kuwahamisha kwa nguvu katika shamba hilo na kubomoa nyumba zenu.

Akizungumza na gazeti hili jana, dalali huyo alishikilia msimamo kuwa kama kuna maongezi au wananchi wanatarajia kuwa na mazungumzo na mwenye eneo hilo, wayakamilishe ndani ya muda huo.

“Mimi natekeleza amri ya kukazia hukumu,” alisema.

Makwale alisema kama kutakuwa na makubaliano, ni lazima yasajiliwe kisheria na kwamba ili kuepuka nyumba kubomolewa waingie makubaliano na mmiliki.

Muda huo ulianza kuhesabiwa Novemba 17 wakati Serikali ikiwa imeanza kukusanya taarifa kujua idadi ya wananchi waliopo eneo hilo na idadi ya nyumba.

Katika kesi ya msingi, watawa hao walidai kuwa kati ya mwaka 1993 na 2004, wadaiwa waliingia bila ruhusa katika shamba lao la Kilari na kujigawia eneo la eka 300 na kuanza kulima na kujenga.



Chanzo: mwananchi.co.tz