Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi 3,600 wa Lindi kunufaika na mradi wa maji

Fraesrdtt Wakazi 3,600 wa Lindi kunufaika na mradi wa maji

Sun, 7 Apr 2024 Chanzo: Mwananchi

Zaidi ya wakazi 3,600 katika wilaya ya Lindi mkoani hapa watanufaika na mradi wa maji kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) wenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni.

Hayo yamebainishwa Aprili 7, 2024 na kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Lindi, Mhandisi Atanasi Lume wakati akikabidhiwa mabomba ya maji na mkuu wa wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga.

Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kwamba mradi huo wa maji utagharimu zaidi ya Sh1 bilioni na utakwenda kuhudumia kijiji cha Nanjime Mkwajuni chenye vitongoji sita.

“Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 46 na ujenzi wa tenki unaendelea upo hatua ya uchimbaji wa msingi na upangaji wa mawe na ukikamilika utahudumia vitongoji sita vyenye watu takribani 3,600,” amesema Mhandisi Atanasi.

Kwa upande wake Ndemanga ametoa miezi sita kwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha unakamilika kwa wakati.

“Tuliomba wizarani tukapata Sh1 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu, tulimkabidhi mkandarasi Januari kwa maelezo kuwa ikifika Juni uwe umekamilika, na sasa tumefika nusu ya mradi. “Maeneo haya yana shida ya maji, ardhini yapo juu tu ukichimba unayapata ila hayana ubora kwa matumizi ya binadamu, ndiyo maana tumekuja na mradi huu.

“Niwatake Ruwasa na mkandarasi kuanzia sasa muanze kuhangaika ili tupate pampu na muanze kuwasiliana na Shirika la Umeme (Tanesco) ili tupate umeme, msisubiri wamalize ndipo muanze, tutawachelewesha wananchi kupata huduma hii. Pia, wananchi hii miundombinu ina gharama kubwa, tuitunze na tutunze chanzo chetu cha maji na sio kwenda kulima,” amesema Ndemanga.

Mkandarasi wa mradi huo, Mhandisi Respcious Kabyemela amesema atajitahidi ifikapo Mei 30, mwaka huu, mradi huo uwe umekamilika ili wananchi wapate maji ya uhakika.

“Niahidi mbele ya viongozi wote, ifikapo Mei 30, mradi huu wa maji wa Nanjime Mkwajuni utakuwa umekamilika na wananchi wanapata maji,” amesema Respcious.

Diwani wa kata ya kitomanga, Zuhura Matindila amesema shida ya maji katika kijiji chake ni ya muda mrefu, wanaishukuru Serikali kwa kuwapatia mradi mkubwa wa maji ili kuondoa tatizo hilo .

“Maji yapo lakini sio mengi ya kusambaa Mkwajuni na Kitomanga, tukiyapata haya tutaenda kumaliza tatizo katika vijiji vya Mjimwema na Magereza, naishukuru Serikali na mkandarasi aende na wakati kama alivyosema,” amesema diwani Matindila

Mariamu Salumu, mkazi wa kijiji cha Nachime Mkwajuni amesema kuwa mradi huo utasaidia kuondoa changamoto katika maeneo yao, kwani kwa sasa wanatumia maji ya visima ambayo si salama sana kwa matumizi.

Chanzo: Mwananchi