Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wakazi 18,000 Buhigwe wanafaika na mradi wa maji

Wakazi 18,000 Buhigwe Wanafaika Na Mradi Wa Maji Wakazi 18,000 Buhigwe wanafaika na mradi wa maji

Fri, 10 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (Ruwasa) wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma,imekamilisha ujenzi wa mradi wa maji unaowanufaisha zaidi ya wakazi 18,000 wa vijiji vya Kavomo, Buhigwe, Mlela na mji wa Kiserikali wa Bwega.

Kaimu meneja wa Ruwasa wilaya ya Buhigwe Fransis Mollel alisema,mradi huo uliopo katika kijiji cha Songambele na umegharimu Sh.bilioni 1.62 na ulianza kutekelezwa mwezi mei mwaka 2022 na ulitakiwa kukamilika mwezi Februari 2023, lakini kutokana na sababu mbalimbali umekamilika mwezi Juni.

Alitaja kazi zilizofanyika katika mradi huo ni ujenzi wa tenki kubwa la lita 500,000,ukarabati wa matenki mawili ya lita 90,000 kila moja,ujenzi wa vituo vya kuchotea maji,kuchimba mitaro na kulaza mabomba ya kusambazaji maji kutoka kwenye chanzo hadi kwenye matenki na kwenye makazi ya watu.

Mollel alisema, awali katika vijiji hivyo kulikuwa na miradi ya maji,lakini kutokana na ongezeka la watu hasa katika mji wa Kiserikali wa Bwega miradi hiyo ilizidiwa,hivyo serikali ikaona ni vyema kujenga mradi mpya ambao utatosheleza mahitaji ya maji kwa watu waliopo.

Kwa mujibu wa Mollel,sasa wananchi wa vijiji hivyo wanapata huduma ya maji safi na salama kwa masaa 24 na wameondokana na kero ya kwenda kutafuta maji ya visima vilivyochimbwa kwa mikono ambayo hayakuwa safi na salama.

Aidha alisema,wamekamilisha mradi mwingine wa maji wa Migongo kata ya Kilelema kwa gharama ya Sh.milioni 963 ambao umehusisha ujenzi wa vituo 19 vya kuchotea maji,ujenzi wa tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 100,000 na kufunga umeme jua(solar power).

Pia alisema,wanatarajia kupanua mradi huo ufike hadi kijiji cha Kilelema ambako ni makao makuu ya kata ili wananchi wa kijiji hicho ambao hawana maji ya uhakika waweze kunufaika na matunda ya serikali yao ya awamu ya sita.

Katika hatua nyingine Mollel alisema,wameanza kutekeleza mradi mkubwa wa Nyakimue-Mnanila wenye thamani ya Sh.bilioni 8.2 utakaonufaisha jumla ya vijiji 8 vya Usagara,Mkatanga,Kibande,Bweranka,Kibwiga,Kitambuke,Nyakimwe,Mhanila ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 43.

Mkazi wa kijiji cha Songambele wilayani humo Yunifrida Gobosi alisema,kabla ya mradi huo kujengwa alitumia zaidi ya masaa 2 kwenda kutafuta maji kwenye mito na visima yaliyopatikana umbali wa kilomita 1 kwa ajili ya matumizi ya familia yake.

Mkazi mwingine Pendo Tamu alisema,mradi huo umesaidia sana kuimarisha na kumaliza migogoro ya ndoa iliyotokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa wanawake kuchelewa kurudi nyumbani kila wanapokwenda kutafuta maji.

Ameishukuru serikali kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira Ruwasa, kukamilisha mradi huo uliomaliza mateso ya kutembea umbali mrefu na kero ya huduma ya maji katika kijiji hicho.

Mwanafunzi wa shule ya msingi Songambele Julieth Ayubu alisema,ukosefu wa maji ulisababisha wakose baadhi ya vipindi darasani kwa kuwa wakati mwingine walitakiwa kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya shule hasa suala la usafi wa mazingira na kupikia chakula cha mchana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live