Poilisi mkoa wa Njombe imethibitisha kifo cha Golden Doglas Luoga (34) aliyekuwa mfanyabiashara wa miamala ya fedha katika halmashauri ya mji wa Njombe kilichotokea wakati akiendelea kupata matibabu baada ya kupigwa risasi na watu wawili wanaodaiwa kuwa ni majambazi waliomvamia nyumbani kwake katika eneo la Galuhenga lililopo katika mtaa wa Kmabarage.
Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe John Makuri Imori amesema wamepata taarifi za kifo cha Golden Luoga mapema alfajiri ya leo wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya Mbeya alikohamishiwa kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa wa Njombe.
"Tarehe 29 mwezi wa nane mwaka huu majira ya saa mbili na na dikika arobaini usiku kule katika mtaa wa Kambarage majambazi wawili waliokuwa na silaha za moto waliwavamia Golden Luoga sasa pale kwake alikuwa pia na ndugu yake anaitwa Faraja Luoga yeye ana miaka arobaini"amesema Makuri
Kamanda Makuri ameongeza kuwa; "Kwa hiyo baada ya kuvamiwa pale ndani ndugu hawa wote wawili walijeruhiwa kwa rasasi na wakati wanakimbizwa hospitali siku hiyo hiyo bwana Faraja alifariki lakini Golden yeye akawa anaendelea vizuri na alihamishwa kutoka kwenye hospitali yetu hapa na kupelekwa kwenye hospitali ya rufaa Mbeya lakini alfajiri ya leo tumepata taarifa kwamba naye amefariki," aliongeza RPC.
Aidha, Makuri ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuwa watulivu na kuviamini vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuwa vitawatafuta watuhumiwa popote walipo mpaka watakapopatikana ili sheria ichukue mkondo wake.