Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajawazito wapigwa marufuku kuonekana vilabuni Iringa

Wajawazito Pic Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego

Wed, 26 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amewaagiza wanawake wote kuwa wasimamizi na walinzi, kwa kuhakikisha wajawazito hawanywi pombe kwani ndio sababu ya kuzaa watoto wenye udumavu na magonjwa mengineyo.

Dendego ameyasema hayo kutokana na tatizo la udumavu kuonekana bado ni changamoto mkoani humo.

Amesema suala la lishe duni ndilo linamsikitisha Rais Samia Suluhu Hassan na kwamba wanawake wote ni marufuku kuonekana vilabuni wakinywa pombe kama njia ya kutokomeza magonjwa yanayosababiswa na ukosefu wa lishe.

Dendego ameeleza kwamba agizo hilo linalenga kuleta utambuzi kwa kina-mama kuhusu athari za kunywa pombe wakati wa ujauzito na kuzuia tabia hiyo hatari kwani inaweza kuleta athari kwa mtoto atakayezaliwa.

''Ni marufuku mama mjamzito kuonekana kilabuni ameshikiria bakuli la ulanzi, huo ulanzi ndio unaotengeneza utapiamlo kutoka kipindi mtoto yupo tumboni mpaka kufikia miezi tisa, kina mama na kina baba tushirikiane tuache tabia za hovyo kwani Iringa ni safi ila dosari ni hiyo moja tu,''Amesema Dendego

Dendego amefafanua kuwa kina mama wengi wanatumia pombe aina ya ulanzi na wengine wanachukua hatua ya kuwanywesha hata watoto wadogo na kwamba ongezeko la matumizi ya ulanzi miongoni mwa wanawake wajawazito katika mkoa wake na kuwaomba viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini na Serikali kuwa walinzi na wapambanaji wa suala la udumavu.

Dendego aliongezea kwa kuwaomba kina mama wajawazito kuwa makini na kutotumia pombe kabisa wakati wa ujauzito wao na alisisitiza kwamba kina baba nao wawe msaada katika kuhakikisha agizo hili linatekelezwa kikamilifu.

“Afya ya mama na mtoto ni muhimu sana kwa maendeleo ya mkoa wetu tunahitaji kushirikiana vyema ili kuhakikisha hakuna mama mjamzito anayeenda kilabuni kunywa ulanzi, akikamatwa namfungia mpaka miezi tisa itimie na ajifungue ili kuokoa afya ya mtoto,'' amesema Dendego.

Hata hivyo Dendego alifafanua kwamba Mkoa wa Iringa unatakiwa kuangalia kina mama wote wajawazito wawe salama na kutoa watoto wenye afya njema ,wazaliwe na kilo zinazohitajika lakini pia kina baba pia kuwa walinzi wa familia na kuwajibika kwa afya ya mama na mtoto.

Kwa upande wao wananchi wa Mkoa wa Iringa, kwa nyakati tofauti amekiri kuwa suala la pombe kipindi cha ujauzito si tu kuwa ni changamoto inayosababisha udumavu, lakini pia huleta changamoto nyingine za kiafya.

Baadhi ya wananchi hao wameunga mkono RC Dendego na hivyo kuahidi kuwa watasaidia kuhahakikisha kuwa tatizo la udumavu linalosababishwa na changamoto ya unywaji wa pombe, linaisha na kufanya Iringa kuwa safi.

"Ni kweli wajawazito wanakunywa pombe na mda mwingine hata wakijifungua wanawapa pombe hizo hata watoto," amesema Shida Mahenge, Mkazi wa Kijiji cha Itona mkoani Iringa.

Chanzo: Mwananchi