Wajasiriamali wa Kanda ya Kaskazini wamepata elimu inayohusu namna bora ya upatikanaji wa mitaji na uandaaji wa miongozo ya ushiriki katika mitaji halaiki kupitia Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).
Akizungumza kwenye semina ya kuwezesha wajasiriamali hao iliyofanyika jijini hapa, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa mamlaka hiyo Charles Shirima, amesema: “Hii ni elimu mpya kabisa kwa wajasiriamali wengi.”
Shirima amesema CMSA imeanza mpango mkakati wa kutoa elimu ya kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati namna ya kuandaa miongozo ya upatikanaji wa mitaji halaiki kwa lengo la kuwekeza ili kujiinua kiuchumi.
"Lengo letu ni kuhakikisha wajasiriamali wa kati na wadogo wanapata elimu ya upatikanaji wa mitaji lakini pia kuhusu uandaaji wa miongozo ya ushiriki katika mitaji halaiki," amesema Shirima.
Amesema mfumo huo utasaidia kusimamia biashara ndogo na kati na utasaidia kukusanya fedha za mitaji ya biashara ndogo na kati kwa ajili ya shughuli za uwekezaji kwa kupitia mifumo itakayokuwa inasimamiwa na CMSA.
“Hapa nchini mfumo huu ni mpya, haukuwepo hapo awali, hata hivyo tumeanza kutoa leseni katika kipindi hiki huku wenzetu nchi jirani walianza muda mrefu, na kwamba ni moja ya utekelezaji wa sera za serikali katika kuwezesha wafanyabiashara wadogo na wakati, kupata mitaji na hivyo kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi,” amesema, na kuongeza;
"Kwa hiyo tuna matumaini kwamba kwa kutoa elimu hii itawasaidia wawekezaji wadogo na wakati katika kukuza biashara zao kitu ambacho kitasababisaha ukuaji wa mapato yao binafsi, lakini pia ukuaji wa pato la taifa.”
Mmoja wa wakufunzi wa Taasisi ya Elimu ya Biashara kwa Vijana na Uwekezaji (ICESA- Africa) Geofrey Julius amesema fursa hiyo mpya itaongeza chachu katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali hali ambayo itaruhusu vijana kujiajiri na kuwa suluhisho la upatikanaji wa mitaji.
Mshiriki wa mafunzo hayo Baraka Gaspa ametoa wito kwa vijana kuwa ni vyema wakafuatilia mamlaka hiyo ili kupata taarifa sahihi za uwekezaji kwa lengo la kujiendeleza kiuchumi.
Mshiriki mwingine wa mafunzo hayo Regina Mlay wa jijini Arusha, amesema mafunzo hayo yatawasaidia katika kuwajenga na kujiimarisha kiuchumi kwani awali hawakuwa na elimu hiyo ya uwekezaji.