Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wajasiriamali Mbarali wakopeshwa mil 353/-

8e75c3f81b4fd24005f6cd0edf21c834 Wajasiriamali Mbarali wakopeshwa mil 353/-

Tue, 1 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imetoa mikopo ya Sh 353,550,000 kwa wajasiriamali wanawake, vijana na walemavu katika mwaka wa fedha 2019/2020.

Kiasi hicho cha fedha ni asilimia 10 ya Sh 3,535,500,000 zilizotarajiwa kukusanywa na halmashauri hiyo zikiwa ni mapato ya ndani katika mwaka huo wa fedha.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kivuma Msangi, Idara ya Maendeleo ya Jamii ilisimamia utoaji mikopo kwa vikundi kwa mgawanyo wa asilimia nne ya fedha hizo kwa wanawake, asilimia nne nyingine kwa vijana na asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu.

Msangi alisema, katika kipindi hicho vikundi 37 vya wanawake vyenye wanufaika 680 vilipata mikopo ya jumla ya Sh 141, 420, 000.

Vikundi 29 vya vijana vyenye wanufaika 225 kati yao wakiwemo wanaume 140 na wanawake 85 vilipata mikopo ya jumla ya Sh 141,420,000 na Sh 70,710,000 zilitolewa kwa vikundi 15 vya watu wenye ulemavu vyenye wanufaika 125 wanaume wakiwa 70 na wanawake 55.

Msangi alisema kumekuwa na mwamko mkubwa wa vikundi vya wajasiriamali wilayani humo kuchangamkia mikopo inayotolewa na halmashauri hatua inayoonesha wananchi wametambua nia ya serikali ya kuwawezesha ili kumaliza umasikini.

Hata hivyo, alisema kumekuwa na changamoto zinazokabili juhudi za utoaji mikopo ikiwemo hali ya hewa.

Msangi alisema vikundi vingi vinavyopewa mikopo hujishughulisha na kilimo cha mpunga ambacho hutegemea hali ya hewa hivyo wakati mwingine husababisha mavuno duni na kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati.

Changamoto nyingine ni wingi wa vikundi vya wajasiriamali wakati makusanyo ya halmashauri ni kidogo hivyo kusababisha malalamiko kwa vinavyokosa.

Alisema pia vipo baadhi ya vikundi ambavyo miradi yake ni midogomidogo ambayo matokeo yake hayaonekani kwa urahisi hivyo kusababisha ugumu kuvifanyia tathmini na kuvipa mikopo ili viweze kunufaika sawa na vingine.

Msangi alisema halmashauri hiyo inaendelea kuhamasisha vikundi vya wanawake kubuni miradi isiyotegemea mabadiliko ya hali ya hewa ukiwemo ufugaji kuku, mbuzi, nguruwe, ufumaji na uanzishwaji wa viwanda vikiwemo vya kusindika maziwa, nyama na mboga.

Mkakati mwingine ni kuimarisha ufuatiliaji wa mara kwa mara kwa kila hatua za utekelezaji wa shughuli za vikundi sanjari na kuviunganisha na wataalamu kwa ajili ya kuwapa ushauri ili kufikia malengo.

Chanzo: habarileo.co.tz