Kisarawe. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), nchini Tanzania, Mwita Waitara ametoa siku 14 kwa uongozi wa wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani kuhakikisha wanawakamata na kuwafikisha mahakamani, wale wote waliowapa mimba wanafunzi.
Waitara ametoa agizo hilo leo Jumanne Desemba 17, 2019 wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya kupinga mimba za utotoni, iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni( Unesco).
Waitara ambaye amezindua kampeni hiyo kwa niaba ya Waziri wa Tamisemi, Seleman Jaffo alifikia hatua hiyo baada ya kupewa ripoti ya hali ya mimba kwa wilaya hiyo kutoka kwa mkuu wa wilaya hiyo, Jokate Mwengelo.
Mwengelo alisema katika kipindi cha Januari hadi Oktoba, 2019, wanafunzi 40 waligundulika kuwa na mimba huku watu wanane pekee ndiyo wamefikishwa mahakamani.
Amesema kati ya wanafunzi hao 40 waliopewa mimba, wanafunzi 38 ni wa shule za sekondari huku wanafunzi wawili wakiwa ni wa shule ya msingi.
Alisema moja ya changamoto iliyopo ni baadhi ya wazazi kushindwa kutoa ushirikiano kwa watu waliowapa mimba wanafunzi .
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Waitara alisema ametoa wiki mbili kuhakikisha watu waliohusika kuwapa mimba wanafunzi hao wanatafutwa sehemu walipo na kufikishwa mahakama ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
"Natoa wiki mbili kwa uongozi wa wilaya uwatafute wale wote waliowapa mimba wanafunzi hawa na kuwafikisha mahakamani, kwa sababu watoto wamepoteza elimu yao wakati Serikali inaingia gharama kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi Sekondari" amesema Waitara na kuongeza.
Akitoa taarifa ya hali ya mimba za utotoni kwa Tanzania, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkuu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Anna Mhina, alisema asilimia 27 ya wasichana wenye umri wa miaka 15 walipata ujauzito kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.
Mhina aliitaja pia mikoa inayoongoza kwa kuwa na kiwango cha juu cha mimba za utotoni kuwa ni Katavi yenye asilimia 45, (Tabora (43%), Morogoro (39%), Dodoma (39%) na Mara (37%).
Naye, mwakilishi wa Unesco, Mathias Herman alisema Shirika hilo linatekeleza kampeni hiyo kwa ajili ya kuvunja ukimya dhidi ya wanafunzi.