Tanga.Waislamu wa Jiji la Tanga leo wameungana na wenzao Duniani katika swala ya Idd El Fitri huku wakionywa kutokubali kutamka maneno yanayodai kuwa uongozi wa Rais John Magufuli umesababisha hali ngumu ya maisha.
Wameelezwa kwamba maeneo hayo hayapaswi kuzungumzwa na Waislamu kwa sababu yanapingana na maelekezo ya Mwenyezi Mungu ambaye ameelekeza kwamba wanapoona maisha magumu wanatakiwa kujitafakari juu ya matendo yao.
Maelekezo hayo yametolewa leo Juni 15 na Sheikh Salim Bafadhili wakati akitoa hotuba ya swala ya Idd El Fitri iliyoswalishwa na Ustaadh Amin Said (Ammy) katika uwanja wa Tangamano Jijini Tanga
"Msizitukane zama hakika zama ni Allah mwenyewe,"alisema Sheikh Bafadhil wakati akinukuu maneno kutoka katika kitabu kitakatifu cha Quran
Aliwataka waislamu wasilalamikie hali ngumu badala yake wajikite katika kufanya ibada na kuepuka maovu ili Mungu awape wepesi katika upatikanaji wa riziki.
Sheikh huyo aliwataka wasilamu kusoma vyema dini yao ndipo watakapobaini kwamba hata walioishi zama za nyuma kuna wakati walikumbana na maisha magumu baada ya kukiuka maandiko ya Mungu lakini waliporejea kwenye ibada ya kweli neema ilirejea.
Kuhusu Sikukuu ya Eid,Sheikh huyo aliwahimiza wanawake kuimarisha mema waliyokuwa wakiyafanya wakati wa mwezi wa Ramadhani ikiwamo kuvaa mavazi ya kuwasitiri ili amani na utulivu uliokuwepo uendelee.
Katika msikiti mkuu wa Ijumaa jijini Tanga,Sheikh wa baraza kuu lawaislamu (Bakwata) Mkoa wa Tanga,Juma Luwuchu aliwaeleza wasilamu kwamba Mwenyezi Mungu waliyekuwa wakimnyenyekea mwezi wa Ramadhani yupo miezi yote.