Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waingiwa hofu mafuriko kaya 106 zikikosa makazi

MAFURIKO Waingiwa hofu mafuriko kaya 106 zikikosa makazi

Mon, 4 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KAYA 106 zenye watu zaidi ya 400 katika Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera, hazina mahala pa kuishi baada ya nyumba zao kujaa maji kutokana na mvua inayoendelea kunyesha.

Kutokana na tatizo hilo, wananchi hao wamepewa hifadhi katika Shule za Msingi S.K. na Omundongo zilizoko katika wilaya hiyo, hadi makazi yao yatakapokuwa salama.

Wakizungumza na Nipashe jana, baadhi ya wananchi walioathiriwa na mafuriko hayo akiwamo Lucia Mkagaruki, walisema walizingirwa na maji na wakashindwa kuvuka hadi askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji walipokwenda kuwaokoa na kuwapeleka eneo salama.

"Askari walipofika, wakawa wanatuita tuvuke, hatukuweza maana maji yalishakuwa mengi, walilazimika kuja kutuvusha na watoto wetu tukapelekwa ng'ambo ya pili, lakini mali zetu zote zilibaki huko, wasingeweza kutuvusha sisi na mizigo yetu," Lucia alisimulia.

Mwathirika mwingine wa mafuriko hayo, Erica Johnbosco, alisema wanashukuru kwa kuokolewa na kupewa hifadhi na serikali, lakini hofu yake ni kutokuwa na chakula pale mvua itakapokwisha na wao kurejea katika makazi yao.

"Mazao yote yameharibika, tulikuwa na migomba, mihogo, viazi, magimbi na mengine, lakini yote yamemezwa na maji, hatujui tutakula nini tukirejea nyumbani," alisema.

Naye Johnbosco Benedicto alisema kuwa baada ya kupewa hifadhi katika shule, kila chumba kimoja cha darasa zinakaa familia nne na kuwa wanalala kwa kuchanganyikana na watoto wao.

"Wataalamu wa afya kutoka halmashauri walikuja wakatupa elimu namna gani tujikinge na ugonjwa wa corona, tumepewa ndoo na sabuni, tunanawa ili kuhakikisha tupo salama," alisema.

Ili kuhakikisha wanaendelea kuwa salama, wadau mbalimbali likiwamo Shirika la World Vision Tanzania wameendelea kujitokeza kuwasaidia kupata mahitaji mbalimbali yakiwamo ya chakula.

Akikabidhi msaada wa unga kilo 1,600, maharage kilo 320, mablanketi 248, vyandarua 200 na dawa ya kutibu maji vidonge 120,000 vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 16.7, Mwakilishi wa Meneja wa World Vision Kanda ya Kagera, Victor Nsiima, aliwataka kutoviuza na badala yake wavitumie kama ilivyokusudiwa.

"Vitu hivi mnavyoviona vimetolewa kwa moyo ili viwasaidie, msiviuze maana kufanya hivyo mtawakatisha tamaa watu wenye nia ya kuwasaidia," alionya.

Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Denice Mwila, aliwataka wananchi waliojenga mabondeni, kuhama na wenye nia ya kujenga katika maeneo hayo kuacha, ili kuepuka madhara yanayoweza kuwakumba wakati wa msimu wa mvua.

Kanali Mwila alisema wananchi walioathiriwa zaidi na mvua hizo ni kutoka vijiji vya Mabuye, Omundongo, Kasambya na Burifani, na mbali na wananchi zaidi ya 400 kuhifadhiwa katika shule hizo, wengine wamepata hifadhi kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live