Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahojiwa na polisi undani wa anayedaiwa kuuawa na mkewe

Msele 4959034 Mfanyabiashara wa Mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, Evagro Msele aliyeuawa na mke wake Beatrice.

Tue, 28 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watu kadhaa wanahojiwa akiwamo mwanamke anayedaiwa kuwa chanzo cha mgogoro uliosababisha mauaji ya mfanyabiashara wa Mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, Evagro Msele.

Mfanyabiashara huyo (43) anadaiwa kuuawa na mkewe, Beatrice Elias (36), mkazi wa Mtaa wa Katanini, Wilaya ya Moshi saa tatu usiku wa Mei 25 mwaka huu huko katika Kitongoji cha Pumuani A, Kata ya Kirua Vunjo baada ya kumkuta kwa mzazi mwenzake.

Wakati mwanamke huyo (jina limehifadhiwa) akiendelea kuhojiwa na Jeshi la Polisi kuhusiana na tukio hilo, Nipashe jana ilifika nyumbani kwa Msele ulikowekwa msiba, ilishuhudia babu wa marehemu (jina tunalo), akielekeza watoto sita wa marehemu wajiandae kwenda kumwona mama yao mahabusu.

Jana, Philip Msele, mjomba wa marehemu wakati anatoa taarifa ya familia kwa waombolezaji, alisema mwanamke anayehojiwa alikuwa amezaa na marehemu mtoto mmoja mwenye umri wa miaka saba.

Philip alisema tayari polisi wamekabidhi mwili wa ndugu yao kwa familia kwa ajili ya kuendelea na taratibu za mazishi.

“Leo (jana) tulikwenda pale Kituo Kikuu cha Polisi Moshi saa mbili asubuhi na tukaelekezwa kwenda pale KCMC (Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Kaskazini) na uchunguzi umefanyika chini ya madaktari, polisi na familia.

"Ni kweli Evagro Michael Msele ana watoto saba, sita kwa mke wa ndoa (Beatrice) na huyo mwingine, ana mtoto naye mmoja mwenye umri wa miaka saba. Msele atazikwa nyumbani kwake Mtaa wa Katanini, Kata ya Msaranga, Manispaa ya Moshi," alisema.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, mke wa ndoa Beatrice, alimvizia mumewe akitoka nyumbani kwa mzazi mwenzake na kumchoma na kitu chenye ncha kali. Juzi Kamanda Maigwa alisema wanamshikilia Beatrice kwa mahojiano zaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live