Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahofia kubeba mimba kisa zahanati

Kupandikiza Mimba (600 X 468) Wahofia kubeba mimba kisa zahanati

Wed, 15 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakazi wa kijiji cha Ivilikinge wilayani Makete Mkoa wa Njombe wameeleza uamuzi wao wa kutobeba mimba kwa sababu ya kukosa huduma za uhakika za matibabu katika kijiji hicho

Wametoa kauli hiyo mbele ya mkuu wa wilaya ya Makete, Juma Sweda wakati akipokea msaada wa mabati 200 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho uliotolewa na benki ya NMB.

Wamesema zahanati iliyopo sasa ni chakavu na miundombinu duni iliyojengwa zamani kiasi cha kushindwa kuendana na mahitaji ya sasa ya utoaji huduma za afya hasa za uzazi salama.

Wamebainisha kuwa jengo la zahanati hiyo ni dogo ambalo linasababisha mrundikano wa wagonjwa wengi hadi wengine kukosa sehemu ya kupumzishwa baada ya kupata matibabu.

Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wakiwemo Abia Sanga, Amokile Mgaya na Yona Tweve wamesema ilifikia hatua wajawazito ni wengi katika zahanati lakini vyumba ni vichache hali iliyowafanya kuchukua uamuzi wa kujenga zahanati kubwa itakayokidhi mahitaji yao.

"Kuanzia sasa sisi wanawake tuhamasishane kuzaa kwa kuwa jengo hili la zahanati inayojengwa sasa itakidhi mahitaji na tutajifungua salama," amesema Sanga.

Advertisement Mkuu wa wilaya ya Makete, Juma Sweda mara baada ya kupokea msaada huo wa mabati ambayo thamani yake ni Sh8.5 milioni amesema utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa zahanati utafanyika haraka iwezekanavyo ili wananchi  wa kijiji hicho waweze kunufaika na huduma  za afya.

Aliiomba benki hiyo kutoa msaada mwingine wa vitanda ili kuboresha zahanati na wakina mama waanze kushika mimba na kujifungua katika mazingira salama.

"Kwa kuwa zahanati hii itaisha niwaombe mtuongezee vitanda na tukishafanya hivyo wakina mama wapo wanataka kujifungua na wapo tayari kushika mimba "amesema Sweda.

Meneja wa Benki ya NMB kanda ya Nyanda za juu kusini, Straton Chilongola amesema walipopata maombi ya kuchangia maendeleo katika wilaya hiyo walifarijika na kuamua kushiriki katika kuchangia kwenye sekta hiyo muhimu katika jamii.

"Vifaa hivi tunavyokabidhi leo ni moja ya ushiriki wetu katika maendeleo ya jamii na tunao wajibu wa kuhakikisha kuwa jamii inayotuzunguka inafaidika na faida tunayoipata," amesema Chilongola.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live