Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahitimu ESAMI watakiwa kuwa chachu ya maendeleo barani Afrika

Mon, 26 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka wahitimu wa Taasisi ya Mafunzo ya  Uongozi na Utawala katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAMI) kuwa chachu ya maendeleo barani Afrika.

Akizungumza katika mahafali ya ESAMI leo Jumamosi Novemba 24, 2018 iliyoshirikisha wahitimu kutoka mataifa 22 barani Afrika, Profesa Ndalichako amesema Bara la Afrika linahitaji viongozi ambao wataleta mabadiliko.

"Hiki chuo muhimu sana katika kuchochea mabadiliko katika fani mbalimbali barani Afrika kwani bado kuna changamoto ya uadilifu kwa viongozi, rushwa na ubinafsi," amesema

Amesema kwa kuwa wahitimu wengi wa chuo hicho ni wafanyakazi waliopo kazini katika taasisi mbalimbali, wana fursa nzuri kuchochea maendeleo katika maeneo yao.

Baadhi wa wahitimu wa chuo hicho, akiwamo Mhariri Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu na diwani wa viti maalum (Chadema) Viola Likindikoki wamesema elimu ambayo wameipata watakwenda kuitumia kuchochea maendeleo katika sehemu zao.

Machumu aliyehitimu shahada ya uzamili amesema Afrika inakabiliwa na changamoto kubwa kama yalivyo mabara mengine zikiwamo za kibiashara na kiutendaji.

Hata hivyo, amesema  Afrika haiwezi kutegemea watu wengine kujikomboa inatakiwa kujisimamia kwa kutengenezea wataalamu wake wenyewe wa kujikomboa.

"Tumepata elimu, lakini cha pili ni kujipanga tunakwenda kuifanyia nini Afrika,” amesema Machumu.

Kwa upande wake Likindiko amesema elimu ambayo wameipata wataitumia kusaidia taasisi zao kutatua changamoto zinazowakabili.

"Kuna maswala ya uadilifu ikiwamo rushwa, tutajitahidi kwenda kukabiliana nayo ili kuchochea maendeleo katika jamii," amesema.



Chanzo: mwananchi.co.tz