Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahamiaji haramu 12 kutoka Ethiopia wakamatwa Manyara

Watu 12 Pic Kamanda wa polisi Mkoani Manyara kamishna msaidizi (ACP) George Katabazi

Wed, 19 Jul 2023 Chanzo: Mwananchi

Raia 12 wa Ethiopia, wanashikiliwa na polisi mkoani Manyara, kwa tuhuma za kuingia nchini bila kibali na kutaka kusafiri kwenda nje ya nchi.

Kamanda wa polisi mkoani Manyara Kamishna msaidizi wa polisi, George Katabazi akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Julai 19, 2023 amesema wahamiaji hao wamekamatwa kijiji cha Chemchem kilichopo kata ya Mtuka wilayani Babati.

Amewataja waliokamatwa ni Kliiu Tekel (18), Chrente Alumu (17), Uglu Tekel (17) Yosef Haile (18), Hoss Teke (18), Baraka Gadafa (17), Marian Arenga (19), Samweli Yemeke (17), Yetham Haile (18), Algeze Arenga (17), Maratu Wotso (18) na Buruk Charine(18).

Amesema watuhumiwa hao walikuwa wanasafiri kwa gari dogo aina ya Toyota Mark X ikitokea mkoani Arusha kupitia barabara kuu ya Arusha-Babati.

"Tulipopata taarifa tuliweka mtego wa kuikamata hii gari hata hivyo dereva wa gari hilo baada ya kugundua kuwa anafuatiliwa alichepuka toka barabara kuu na kuingia barabara ya changarawe kwenda Kijiji cha Chemchem ndipo tuliwakamatia," amesema Katabazi.

Amesema upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea na endapo ukikamilika raia hao wa Ethiopia watafikishwa mahakamani.

Wakati huo huo, polisi inamsaka dereva wa gari aina ya Toyota Noah ambaye hakufahamika jina anayedaiwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi bunda 264 sawa na kilogramu 110 zilizokuwa zimefichwa ndani ya magunia manne ya katani.

Katabazi amesema mirungi hiyo ilikuwa inasafirishwa kwenda Babati kutoka Arusha ila waliweka mtego dereva alipougundua alisimama na kukimbia kusikojulikana.

Amewaonya wamiliki wa magari, madereva kuacha kusafirisha dawa za kulevya na wahamiaji haramu kwa kuwa hawataweza kuvuka salama mkoa huo zaidi ya kukamatwa.

Chanzo: Mwananchi