Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wahalifu wageuka walinzi Mikumi

Operanews1680789790742 Wahalifu wageuka walinzi Mikumi

Fri, 7 Apr 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Vijana waliokuwa wakiongoza kwa vitendo vya ujangili kwenye Hifadhi ya Taifa ya Mikumi mkoani Morogoro, maarufu kama ‘Mapanga Shaa Shaa’,  sasa wamebadilika na kugeuka walinzi wa mbuga hiyo.

Hayo yalibainika mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari walipotembelea mbuga hiyo iliyoko kilomita 288 kutoka jijini Dar es Salaam.

Wahariri hao walikuwa kwenye mafunzo ya siku tatu yaliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari wa Mazingira (JET) yanayofadhiliwa na Internews Earth Journalism Network East Africa.

Akizungumza na Nipashe, Mwenyekiti wa Chama cha Mikumi Environmental Conservation Development (MECODE), Musa Buhaki, alisema vijana hao walikuwa wakiingia kwenye hifadhi hiyo na kukamata wanyama kwa ajili ya kwenda kuuza kama kitoweo kujikwamua kiuchumi.

Buhaki alisema baadhi ya vijana hao walikuwa wakijeruhiwa na wanyama wakali na wengine kufariki dunia lakini kwa sasa baada ya kupata shughuli za kiuchumi wameachana na ujangili huo.

“Kwa sasa huwezi kukuta kijana anaingia kwenye hifadhi kufanya ujangili kwa sababu wenyewe ndio wamegeuka kuwa walinzi wa hifadhi na kila mwananchi anayeishi pembeni ya hifadhi amegeuka kuwa mlinzi kwa hiyo si rahisi kufanya ujangili  kama ilivyokuwa zamani.

“Kwa kweli vijana walikuwa wanaumia sana wengine wadogo sana umri wa watoto wetu walikuwa wanapotea tukaona hili litaendelea mpaka lini tukaanza kuwaita kuwaingiza kwenye shughuli zetu na kuwalipa fedha kidogo kidogo,” alisema.

Alisema baada ya kuanza utaratibu huo vijana hao walianza kuambiana kuhusu shughuli hizo na wengi walianza kukubali kuacha ujangili na kufanyakazi halali ya kusafisha mbuga kwa ujira kidogo.

“Tulianza na vijana wachache lakini kadri siku zilivyozidi kwenda walikuwa wanaambiana na sasa tunakwenda na vijana kuanzia 20 na zaidi tunafanya kazi na kuwalipa kidogo kidogo na wote wamekubaliana na kazi hii. Hawaendi  tena kufanya ujangili wa wanyama,” alisema.

Alisema wamekuwa wakiokota vyuma chakavu wakati mwingine hadi tani moja na kwenda kuviuza na kupata fedha za kutosha kulipa vijana hao Sh 7,000 kila mmoja kwa siku.

Pia alisema kupitia shughuli hizo za usafi wanachama wa kikundi cha MECODE akiwemo yeye wanasomesha watoto wao kwenye vyuo mbalimbali vya elimu ya juu.

Alisema kabla ya kuanza kazi hiyo ya usafi alikuwa akifanya kazi ya uganga wa kienyeji na akifahamika zaidi kama Dk. Kimbunga kwa watu wa maeneo ya Mikumi.

Hifadhi ya Mikumi ambayo inapitiwa na takribani kilomita 50 za barabara inayotoka Dar es Salaam hadi Tunduma imekuwa ikipoteza wastani wa wanyama 700 kila mwaka wanaogongwa na magari.

Hifadhi hiyo inatarajia kuanza kufunga kamera za usalama barabarani ikiwa njia ya kuwadhibiti madereva ambao hawazingatii mwendo wa kilomita 50 kwa saa wanapokatisha kwenye mbuga hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live