Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagorowa na changamoto walizopitia

06dfce1151d0a4cead9a6a94efb7ba6c Wagorowa na changamoto walizopitia

Fri, 12 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAGOROWA ambao pia huitwa Wafiome ni kabila dogo la watu wanaopatikana wilayani Babati na mashariki ya Wilaya ya Hanang mkoani Manyara. Watu wa jamii hii pia wanapatikana kaskazini mwa Kondoa mkoani Dodoma.

Wagorowa ni kundi la jamii ya Wakushi wanaopatikana katika nchi za Ethiopia, Eritrea na Somalia, kama ilivyo kwa Wairaqw, Waalawa na Waburunge.

Asili yao ni kutoka Blue Nile, mto unaoanzia Ethiopia. Kutoka huko walisogea hadi Malangwatay (sasa ni Ziwa Eyasi) lililopo mpakani mwa mikoa ya Manyara na Shinyanga nchini Tanzania.

Hivyo, nchi ya kiasili ya Wagorowa kwa Tanzania ni eneo la Babati Mjini pamoja na eneo linalozungusha Ziwa Babati. Vijiji vya Wagorowa vinaenda magharibi kutoka hapa mpaka Mto Duuru (Mto Bubu), na mashariki mpaka mbuga ya wanyama ya Tarangire.

Hakuna mipaka ya kijiografia, na wazungumzaji wa Kigorowa huishi pamoja na wazungumzaji wa Kimbugwe kwenye vijiji kama Magugu, sehemu za kaskazini na wazungumzaji wa Kirangi na Chasi (Alagwa) sehemu za kusini kama vile Bereko.

Kwa kiasi kikubwa, Wagorowa wa leo ni wakulima wanaofuga mifugo (hasa kondoo, mbuzi na ng’ombe). Mazao muhimu wanayolima ni mtama na mabogamboga.

Ufugaji unashika sehemu muhimu sana kwenye utamaduni wa Kigorowa, na wengi wanajitambulisha kwanza kama wafugaji kabla ya ukulima.

Watawala wa Kigorowa

Mtawala mkuu wa Kigorowa aliitwa “Wawitamo” na chini yake alikuwepo “Gaawsamo” aliyetawala eneo fulani tu. Chini yake alikuwepo “Yaabusmo”, huyu kazi yake ilikuwa kukusanya ushuru na kuitisha mikutano kwa amri ya Gaawsamo.

Chini yake alikuwepo “Booymo” ambaye kazi yake ni kutumwa na wakuu wao kuwakamata wahalifu au wasiolipa kodi.

Kiongozi wa Wagorowa aliitwa Haymu Muhanga. Jamii hii ilitajirika kwa ufugaji na kilimo hata wakawa na kiburi cha wakati fulani kumwomba kiongozi wao awatafutie vijana wa kupigana vita. Kiongozi wao aliposita wakamkamata kijana wake wa pekee na kumficha.

Ili kijana aachiwe, Haymu alimfuata kiongozi wa Wabarbaig, akampa ujumbe huo, kisha kiongozi wa Wabarbaig aliwaruhusu vijana wake wakapigane vita dhidi ya Wagorowa.

Wakiwa na furaha na jazba za kivita Wagorowa wakamwachia kijana wa Haymu, na kiongozi huyo aliukabidhi uongozi kwa kijana aitwaye Nalaa, ambaye asili yake ni ukoo wa Barbojik kutoka kwa Wabarbaig, kwa wosia kwamba: “Ukiona kivuli chako kimesimama katikati ya utosi wa kichwa chako, usimamishe vita kwa fimbo” na kutamka neno “Hoyot” yaani “Basi yatosha”.

Aliambiwa asimame upande wa kaskazini kwenda kusini akinyoosha ile fimbo ya mti unaoitwa “Baghrmo” huku akisema mara nyingine neno “Hoyot” mpaka walipotulia.

Walipotulia akawashauri kwamba vita ile waliyoiomba si ya kupigana bali wafanye kuviziana na kunyang’anyana ng’ombe, na watakaoshindwa watatwaliwa mateka, halafu wenzao watawakomboa kwa ng’ombe.

Hii ni namna ya kupata ng’ombe, si kwa kupigana, na mtindo huo uliendelea na wakawekeana kanuni ya ukombozi kwamba kila mateka atakombolewa kwa ng’ombe saba; majike sita na dume mmoja. Tabia hii ilikoma pale utawala wa wageni uliposhika nafasi ya utawala wa wenyeji.

Kutoka pale Maangwatay, vita vya mara kwa mara viliwafanya watawanyike kwa makundi, maana walichoshwa na vita vya kunyang’anywa ng’ombe na Wabarbaig, ndipo Wairaqw wakaelekea Guse kutambika tambiko liitwalo “Diibu’umo” kwa kutumia kondoo dume mweusi asiye na ila.

Kuanzia hapo hawakuandamwa tena na Wabarbaig. Lakini kundi la pili la Wagorowa wakiongozwa na Nalaa lilielekea hadi Dawar karibu na Mlima Hanang’w na halikufanya tambiko ili vita vikome. Hivyo, waliendelea kupigwa na Wabarbaig wakahama kutoka pale Dawar hadi Mlima Singe au Kwaraa na hatimaye wakafika eneo la Gallapo.

Nalaa akawa maarufu miongoni mwa Wagorowa na akatuma ujumbe kwa Wairaqw kuulizia tambiko lipi walifanya kushinda vita. Waliarifiwa na kutekeleza tambiko na hapakuwa na mapigano tena. Naala aliendelea kuwa mtawala wa Wagorowa na ukoo wake ulipokezana uongozi mpaka uongozi wa sasa uliposhika nafasi.

Nyumba za asili za Wagorowa

Nyumba za asili za Wagorowa zilijengwa kwa miti na ziliezekwa kwa nyasi (msonge). Baadaye walijenga nyumba za tembe zilizofanana na handaki ili kujihami na vita kati yao na Wamasai. Waliacha nyumba zilizoezekwa kwa nyasi kwa kuona zilikuwa zikichomwa moto na adui.

Chakula cha asili cha Wagorowa

Chakula kikuu cha Wagorowa ni ugali wa uwele na mtama mweupe (awaka) au mtama mwekundu (udo) na mboga za majani na maziwa. Nyama ilikuwa adimu zamani na ilipatikana kwa kuwinda porini.

Nyama pia hupatikana kama ng’ombe akichinjwa kwa ajili ya tambiko au kwa ajili ya mgonjwa wa ajali ya kuvunjika mifupa. Wagorowa ni hodari wa kufunga mifupa iliyovunjika na kuirudisha katika hali ya kawaida.

Vinywaji vya Wagorowa

Kinywaji kikuu cha kuwaburudisha ni pombe inayotengenezwa kwa mtama na hunywewa kama kiburudisho na starehe, na wakati mwingine kwa sherehe za ndoa na jando.

Pombe ya harusi hutiwa asali kwa heshima ya wakwe, na kwa heshima ya mtawala au mganga wa jadi siku ya jando. Vilevile pombe ya kumwangukia baba hutiwa asali, na atainywa na ndugu zake wa ukoo na wazee wa rika ake.

Ngoma za asili za Wagorowa

Wagorowa wana ngoma mbalimbali kama “Oowe” ambayo huchezwa wakati mazao ya mwaka yameanza kupevuka; “ayla” ambayo ni kwa ajili ya harusi; na “Heelo” ambayo huchezwa na watu wazima tu.

Pia ngoma ya “Foori” inayochezwa na wanaume kwa ajili ya lalamiko la mmoja wao kufanyiwa tendo la dharau; na kadhalika.

Mavazi ya asili

Wagorowa zamani walivaa ngozi iliyotengenezwa vizuri na kulainishwa. Vazi la kiume ni ngozi ya kutosha kujifunika na lina vitundu vidogo vya kuruhusu hewa. Vazi la mwanamke ni zaidi ya moja. Viatu vya zamani ni vya ngozi za wanyama vilivyotengenezwa kwa kamba za kushikilia miguu.

Mapambo ya asili

Mapambo ya asili ya mwilini ni vikuku vya shaba nyeupe au njano (saxeeni na quturmo, gangalhhamo); vikuku vya pembe za tembo (qamqamay); heleni (usaaqaan na gullani) na shanga za ukubwa mbalimbali.

Wagorowa walitumia rangi ya blue iliyopatikana katika majani fulani kwa pambo la midomo na udongo mweupe kama chokaa kuwapaka mwili mzima vijana walio katika jando.

Vilevile walichanjwa chale katika mashavu kwa mmea uitwao “ningesi”, mistari mitatu kila shavu na walitoboa masikio na kuweka heleni. Pia waling’oa meno mawili ya chini.

Tiba za asili

Wagorowa walitumia mizizi ya miti kama tiba ya magonjwa mbalimbali. Mizizi hiyo ilichemshwa au kupondwapondwa na wagonjwa kunyweshwa maji baada ya kuchujwa.

Mahakama ya jadi

Hukumu zote lazima zifuate kanuni zilizokwisha wekwa, na wenye kutoa hukumu ni wazee, yaani wazee hutoa hukumu kwa kufuatisha uamuzi uliokwisha fanywa na wazee wa zamani.

Pia kuna mahakama ya akina mama endapo jambo linawagusa au linavunja hadhi yao na kukiuka miiko yao na maamuzi yao waliyofanya mbele ya wazee wawakilishi. Lakini hakuna mahakimu rasmi, jambo linapokuwa gumu wataita hata wazee kutoka vijiji vingine.

Faini (Dohho) mbalimbali zilikuwa na viwango visivyobadilika. Endapo mtu ametuhumiwa kosa fulani naye amekana kabisa mbele ya wazee na kosa hilo ni zito, basi mlalamikaji akisema tule kiapo cha laana, hapo wazee watapima uzito wa jambo hilo.

Kama laana itatolewa idhini na wazee basi watafanya hivyo. Kama tuhuma ni ya mauaji wataenda penye kaburi na hapo mlalamikaji na mlalamikiwa watasema maneno ya kuapa na kulamba udongo wa kaburi.

Atasema: “kama namsingizia huyu mtu basi laana inipate” na mtuhumiwa vilevile atasema; “kama nimefanya mauaji haya laana inipate”.

Kwa makosa mengine kinachotumika ni asali ya nyuki katika kiapo. Makosa mabaya sana ni kuiba asali, kuiba zana za chuma, kumrusha mtu ng’ombe wake, hasa ng’ombe wa Mgorowa au Muiraqw na tendo la kujamiiana watu walio ndugu au jamaa wa karibu, na kufanya uchawi kwenye nyumba ya mwingine.

Mbali na adhabu ya kulipa faini ya ng’ombe au mbuzi au kondoo, adhabu nyingine ni kutengwa na jamii, hakuna kusaidiwa lolote au kutembea na watu mpaka mtengwa amekubali kuungama kosa lake au kutafuta “wayda” (amani), adhabu hiyo ni kali sana inaitwa “bayni”. Hii hutumika kwa aliyekana kosa na kukataa adhabu za mila ya Wagorowa.

Malezi ya watoto wa Kigorowa

Mtoto wa Kigorowa anapozaliwa na kukua hufundishwa maadili mema ya kuishi na jamii. Mtoto wa kike hufundishwa na akina mama maadili mema ya kuishi na mume na namna ya kutunza familia anapoolewa na kuzaa.

Mtoto wa kiume hufundishwa na akina baba maadili ya kuishi na jamii, mbinu za kujitegemea katika kutunza familia anapokuwa ameoa.

Sherehe za jando

Wagorowa hufanya tohara kwa watoto wa kike na kiume na sherehe kubwa hufanyika wakati vijana wanapoingia jando na unyago.

Ndoa za Kigorowa

Ndoa za Kigorowa hufanyika kwa makubaliano kati ya waozaji wa mtoto wa kike na wa kiume. Kwa kawaida mahari yanayolipwa ni dume wadogo watatu, kubwa mmoja. Pia vinywaji hunywewa wakati wa sherehe.

Makala haya yametokana na taarifa ya kamati ya tamasha la utamaduni wa Wairaqw na Wagorowa – Wilaya ya Babati.

0685 666964 au [email protected]

Chanzo: www.habarileo.co.tz