Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wagonjwa kipindupindu Mwanza wazidi kuongezeka

Wagonjwa 10 Kutibiwa Mfumo Wa Umeme Wa Moyo JKCI Wagonjwa kipindupindu Mwanza wazidi kuongezeka

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Idadi ya wagonjwa wa kipindupindu imeendelea kuongezeka mkoani Mwanza kutoka wagonjwa 80 siku tano zilizopita na kukaribia kufika 100.

Akizungumza leo Januari 20, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa amesema kwa sasa wagonjwa wanakaribia 100, huku Wilaya ya Nyamagana ikiwa na wagonjwa 50.

Hata hivyo, Dk Rutachunzibwa aliyekuwa akijibu swali la Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi wakati wa mafunzo ya kujikinga na kipindupindu kwa makundi maalum, hakuwa tayari kutaja idadi kamili ya wagonjwa waliothibitika kuugua ugonjwa huo. 

"Miongoni mwa wagonjwa wa kipindupindu walioripotiwa mpaka sasa hivi, watu 15 tulivyowafuatilia tulibaini walipata maambukizi haya wakiwa msibani, hivyo basi niwaombe mnapoenda kwenye misiba hakikisheni mnakuwa na vifaa vya kunawia mikono, lakini pia epukeni kukaa matanga muda mrefu," amesema Dk Rutachunzibwa.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Makilagi mbali na kutoa wito kwa jamii kuwa kila mtu anatakiwa kuwa balozi, amesema kwa jana walipokea wagonjwa wapya 13 huku kifo kikiendelea kusalia kuwa ni kimoja katika Mkoa wa Mwanza.

"Niwaombe watu wote mlioshiriki kupatiwa mafunzo haya mkawe mabalozi kwa wenzenu. Ni aibu kusikia mtu amekula kinyesi kibichi kwa sababu ugonjwa huu unaambukizwa kwa kula kinyesi kibichi chenye vimelea vya ugonjwa huo,” amesema.

Amesema Serikali imejipanga kukabiliana na ugonjwa huo kwa kutoa elimu kwa jamii, tahadhari na kuwahudumia wanaobainika na kuhisiwa na ugonjwa huo.

Naye Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoa wa Mwanza, Renard Mlyakado amesema ugonjwa huo umesambaa katika wilaya nne miongoni mwa wilaya saba za Mkoa wa Mwanza ambazo ni Ilemela, Nyamagana, Magu na Ukerewe.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Yusuph Joram, ameiomba Serikali kuzidi kutoa elimu katika makundi mengine ya jamii ili kupambana na kudhibiti ugonjwa huo.

"Elimu hii ambayo mmetupatia kwa siku ya leo inaenda kuwa na mchango mkubwa sana kwetu na sisi tunaahidi kwenda kushirikiana na Serikali kuhakikisha tunatoa elimu kwa wengine ili kutokomeza mlipuko huu," amesema Joram.

Januari 9, 2024 Mganga Mkuu wa Jiji la Mwanza, Pima Sebastian na Mkuu wa Wilaya ya Magu,  Rachel Kasanda walithibitisha kuwepo mlipuko huo mkoani Mwanza ambapo mtu mmoja alifariki.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live