Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waganga wa jadi wafunguka mauaji ya watoto wa Njombe

40143 Pic+waganga Waganga wa jadi wafunguka mauaji ya watoto wa Njombe

Tue, 5 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kuanzia Novemba mwaka jana hadi sasa yameibuka matukio ya kutekwa, kuuawa kisha kutupwa porini watoto wenye umri wa chini ya miaka 11 wilayani Njombe.

Kushamiri kwa matukio hayo, kumesababisha hofu na sintofahamu kwa wazazi na wananchi kwa ujumla kutokana na chanzo cha ukatili huo kutojulikana.

Hadi sasa si viongozi, vyombo vya dola wala wananchi ambao wamepata majibu ya kujitosheleza juu ya chanzo hasa cha mauaji hayo.

Hali hiyo inazidi kuibua maswali mengi kuliko majibu kutokana na ukatili huo kuwalenga zaidi watoto wenye umri huo.

Kati ya watoto wote waliochinjwa, waliobainika kunyofolewa viungo vya mwilini ni wawili, mmoja wa kiume alinyofolewa sehemu zake za siri na mmoja wa kike aliyekatwa sikio, lakini takribani watoto wote wameonekana kuchinjwa shingoni na kukatwakatwa kichwani na shingoni.

Wapo wanaohusisha ukatili huo na imani za kishirikina kwa misingi ya kutafuta utajiri, pia wapo wanaohusisha matukio hayo na migogoro ya kifamilia, ardhi na visasi. Kwa ufupi kila mmoja amekuwa akifikiri lake.

Tayari Serikali imeshapeleka kikosi kazi maalunu kufanya uchunguzi kwa lengo la kukomesha matukio hayo huku pia ikichukua hatua za kukabiliana na hilo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hammad Masauni alifika mkoani Njombe na kukaa siku tatu akishughulikia tatizo hilo.

Akiwa Njombe, Masauni alikutana na waganga wa tiba asili na machifu wa mkoa huo kwa lengo la kutafuta kiini cha matukio hayo.

Katika kikao kati ya waganga hao na Naibu Waziri Masauni, mambo mengi yaliibuliwa.

Chifu wa Kabila la Wabena mkoa wa Njombe, Elias Mkongwa akizungumza kikaoni hapo alisema matukio hayo kwao ni mageni na ni jambo linaloichafua jamii ya watu wa Njombe na mkoa kwa ujumla.

Chifu Mkongwa anasema licha ya kutofahamika kwa chanzo halisi cha mauaji hayo, lakini wanaona huenda utitiri wa waganga wa jadi wanaoingia mkoani humo unachangia.

“Tunasikitishwa na haya matuko. mkoa wa Njombe kwa enzi na enzi tangu tukiwa mkoa mmoja na Iringa, hatuna historia ya mauaji kama haya, hata yalipoibuka mauaji ya albino, viongozi wa jadi wa Iringa tulijipanga kukabiliana nayo.

“Ndiyo maana maadhimisho ya siku ya kupinga mauaji ya albino mwaka 2008 kitaifa yalifanyikia Iringa kwa kuwa ni mkoa ambao watu wake (albino) hakuna aliyeuawa isipokuwa wale waliokuja kujaribu kutekeleza uhalifu huo wao ndio waliouwa.

“Yote hiyo ilitokana na Serikali kuwa pamoja na sisi viongozi na waganga wa tiba asili, lakini baadaye viongozi wa mkoa wa Njombe walikuja wakavuruga mambo na kuvunja uongozi wetu kwa masilahi yao.

“Wakaanza kuwaingiza waganga kutoka nje ya Njombe na kuwapa leseni za kufanya shughuli za uganga bila hata kutaka kutushirikisha wenyeji.

“Sisi tunaamini hawa ni waganga waliopata wenyeji lakini ndio wanaofanya ramli chonganishi na kusababisha yote haya,” anasema.

Katibu wa Chama cha Waganga wa Tiba Asili na Mbadala (CCWI) Mkoa wa Njombe, Rosta Ndungulu aliwatupia lawama baadhi ya viongozi wa mkoa huo, kwamba walihusika kuvuruga uongozi wao hadi ukavunjwa na kuanza kuwasajili na kupokea waganga kutoka nje kinyemela.

Mlezi wa waganga wa tiba asili mkoa wa Njombe, Antony Mwandulami anasema “Waganga wa jadi ndio tunaonyooshewa kidole kuhusiana na matukio haya, lakini ukweli ni kwamba hakuna kiungo cha binadamu kinaweza kumfanya mtu awe tajiri”.

Anaongeza “Ila niseme sisi waganga tunafahamiana vyema kabisa kwa umoja wetu lakini wale wanaokuja na kupitia kwa viongozi wa Serikali wakapewa leseni ndio tunaweza kusema wanahusika. Tunaamini kama tungeshirikishwa katika utoaji leseni kumjua kila anayetaka leseni kama kweli ni mwenzetu ingesaidia kutoingiza watu wasiojulikana.

Mwandulami anasema licha ya matukio hayo kuonekana yameegemea zaidi kwenye imani za kishirikina, lakini bado kuna sintofahamu juu ya chanzo halisi kwani hata masuala ya migogoro ya kifamilia ardhi na visasi nayo yanatajwa kuchangia.

Anasema “Kwa mfano huyu mwenzetu aliyepoteza watoto watatu ni dhahiri tukio hilo linatokana na mgogoro wa wazazi kwani baba wa watoto hao alikuwa na mgogoro wa muda mrefu na ndugu yake (anamtaja jina). Huko nyuma alinusurika kuchomwa moto kwa kutumia tairi la gari”.

Anasema “Hivyo ni vyema vyombo vya dola katika uchunguzi wenu hili pia mlitizame kwa jicho la karibu”.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Danford Nziku ambaye watoto wake watatu, Godliva (11), Gasper (8) na Giliad (5) walitekwa Januari 20 na kukutwa wamekufa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kisha kutupwa porini Januari 27, mwaka huu.

Nziku alimtaja mmoja wa wanafamilia yake akidai ndiye aliyehusika na tukio hilo kwani walikuwa na ugomvi kwa muda mrefu.

Kauli ya Serikali

Baada ya kusikiliza maoni na malalamiko ya waganga hao, Masauni alimtaka mganga mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk Bumi Mwamasage, kuzungumzia malalamiko ya utoaji leseni za waganga hao.

Katika maelezo yake, Dk Mwamasage alisema huko nyuma kulikuwa na mgogoro kati ya waganga hao na mratibu afya mkoa wa Njombe, Mathias Gambishi lakini hatua zilichukuliwa ikiwamo kumwondoa.

Alisema, “ni kweli kulikuwa na malalamiko hayo, hivyo yule mtu tukamwondoa na baadaye tukawaita waganga wote kwa ajili ya kurejesha hali ya utulivu na umoja miongoni mwetu ikiwa ni pamoja na kuwarejesha viongozi wa zamani. Hata hivyo, kwa sasa tumesitisha utoaji leseni mpya za waganga wa jadi hadi pale tutakapokuwa tumejiridhisha.”

Baada ya hapo, Naibu Waziri Masauni alitoa agizo kwa uongozi wa mkoa wa Njombe kufanya uhakiki wa leseni zote za waganga wa jadi wote waliopo mkoani humo na kusitisha upokeaji waganga wengine.

“Niwahakikishie wananchi wa Njombe kuwa, Serikali haijawahi kushindwa jambo...hakuna mhalifu aliyewahi kutekeleza unyama kama huu na akabaki salama. Vyombo vimeelekeza macho yake hapa hadi pale tutakapokomesha mauaji haya.

“Tunatuma kikosi maalumu kutoka kila kona za nchi yetu kuja kuungana na vyombo vyetu vya hapa Njombe na endapo matukio haya yataendelea kujitokeza na vyombo vyetu hususani jeshi la polisi lipo basi itabidi wahusika wajitafakari upya.”

Wananchi wapigwa butwaa

Tangu kuibuka kwa mauaji hayo wilayani Njombe, wazazi na walezi wanalazimika kuacha shughuli zao nyakati za asubuhi na mchana ili kuwapeleka watoto wao shuleni kisha kuwafuata muda wa masomo unapokwisha.

Mkazi wa Mji Mwema, Edward Mlowe anasema “Tumeingiwa hofu kubwa, kila mzazi au mlezi analazimika kumpeleka mtoto wake shule asubuhi na mchana anakwenda kumchukua. Si watoto tu hata watu wazima pia tunalazimika kufunga shughuli zetu mapema ili kuwahi kurudi nyumbani kwanza kwa usalama wangu binafsi, pili kuhakikisha usalama wa familia.”

Mkazi wa Mgendela, Eda Luvanda anasema bado ni kizungumkuti kujua sababu za kuibuka kwa mauaji ya watoto wao Njombe huku akisisitiza hali hiyo inachangiwa na watu kumsahau Mungu na kujiingiza upande wa shetani.

“Tuzidi kusali na kumrudia Mola wetu, haya mauaji si utamaduni wetu Njombe, hivyo ni vyema tukazidi kusali na kuomba hawa watu waokoke na wamuogope Mungu,” anasema Eda.

Watoto sasa waogopwa

Kutokana na matukio hayo, hivi sasa wananchi wameingiwa hofu kubwa jambo linalowafanya kutotoa msaada wowote kwa mtoto popote atakapoonekana hata akiwa anahitaji kusaidiwa.

Dereva taksi wa mjini Njombe, Bahati Msigwa anasema wameshatangaziwa kwamba ni marufuku kumbeba mtoto yeyote, popote watakapomuona hata kama anahitaji msaada.

Anasema “Watoto sasa tunawaona kama ni sumu, yaani hata ukimuona ananyeshewa mvua, kapigwa na baridi namna gani, wewe mpishe tu endelea na mambo yako, maana ukithubutu kutaka kumsaidia na kuonekana na mtu mwingine ambaye hakufahamu vizuri ujue usalama wako uko shakani sana.”

Aidha, sasa kumeibuka wimbi la wananchi kujichukulia sheria mkononi dhidi ya watu wanaobainika kutofahamika vyema mbele ya wenyeji ambapo tayari watu kadhaa wameuawa katika maeneo tofauti wakidhaniwa ni miongoni mwa wanaohusika na mauaji ya watoto.



Chanzo: mwananchi.co.tz