Wanawake wawili Wafanyabiashara (Machinga) ambao ni Wauzaji wa viatu na nguo Mjini Njombe wamezua taharuki baada ya kuganda ghafla Barabarani huku wakishindwa kusema chochote kwa zaidi ya saa moja huku sababu ikidaiwa kuwa ni imani za kishirikina.
RPC wa Njombe, Hamis Issa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika eneo la Mtaa wa Posta karibu na jengo ilipokuwa Ofisi za TRA zamani huku akibainisha kuwa Wanawake hao ni Wakazi wa Kijiji cha Lupila Wilaya ya Makete lakini wanaishi Mjini Makambako.
RPC amenukuliwa akisema “Njombe ilisimama kwa muda, hawa akina Dada walikuwa wanauza biashara zao mtaani lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida waliganda, macho wakiwa wanaangalia mbele zaidi ya saa moja, baada ya kupata taarifa Polisi walifika na kuwachukua ili kuwafikisha Kituo cha Polisi lakini mmoja kati yao alitamka neno moja tu ‘Yesu’ na kurudi katika hali ileile na kulazimika kuwapeleka Hosptali ambapo Madaktari walibainisha kuwa Watu hao wana hali za kawaida”
"Tulichoamua sasa hapa Njombe Makanisa ya TAG Viongozi wake wamekusanyika kutoka sehemu mbalimbali kwahiyo tukawatoa Hospitali na kuwapeleka Kanisani kuanzia jana ambapo wamefanyiwa maombezi na kurejea kwenye hali zao za kawaida"
Kamanda Issah amewatoa hofu Wananchi Mkoani humo na kutoa wito kwa Watu kuendelea kununua biashara za Wanawake hao kwakuwa jambo hilo linaweza kumpata Mtu yeyote na sasa wamepona na kuchukuliwa na Ndugu zao.