Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafugaji walalamikia manyanyaso katika minada

8b0411c7adadf177990fd1013941ae07 Wafugaji walalamikia manyanyaso katika minada

Mon, 14 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAFUGAJI katika Wilaya ya Manyoni mkoa wa Singida wameiomba serikali kukomesha mara moja vitendo wanavyofanyiwa na askari Polisi na maofisa mifugo vya kuwanyanyasa kwa kuwapiga makofi na kuwatoza faini kubwa wanapokuwa minadani

Kilio hicho cha wafugaji kilitolewa na Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Lisilile, Mgomi Mrisho kwa niaba ya wafugaji wa wilaya hiyo wakati wakitoa kero wanazofanyiwa minadani mbele ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Charles Fussi ambaye alikuwa akipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wafugaji hao kwenye mkutano wao .

Walizitaja kero nyingine wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na kudaiwa vitambulisho vya ujasirimali kitu ambacho siyo haki, aidha kutoshirikishwa na wataalamu wa mifugo kuhusu chanjo husika badala yake wanalazimishwa na wakikaidi hukamatwa na kupewa faini kubwa.

Walisema pia chanjo za mifugo zinazotolewa kwenye wilaya hiyo ni kandamizi kwa kuwa hulazimisha wafugaji kupeleka mifugo yao hata kama imevunjika miguu na wengine haiwezi kutembea na wasipoipeleka hutozwa faini kubwa.

Aidha wafugaji hao wameiomba serikali kukarabati na kujenga majosho ya kuogesha mifugo yao kwa kuwa yaliyopo ni machakavu na yamekuwa kama maonesho na hata yale yaliyopo hayana maji.

Pia wafugaji hao wameiomba serikali kutenga maeneo yao kwa ajili ya malisho ili waondokane na migogoro ya mara kwa mara na wakulima inayohatarisha uvunjifu wa amani kati ya pande zote mbili.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni , Fussi alitaka vitendo vya unyanyasaji kukomeshwa mara moja kwani huo ni udhalilishaji kwa wafugaji ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa serikali katika kukuza uchumi wa wilaya hiyo.

“Uchumi wa wilaya ya Manyoni kwa kiasi kikubwa umebebwa na wafugaji, minada na mauzo ya ng'ombe, hivyo imekuwa ni sehemu kubwa katika kuchangia maendeleo yake na kuisababishia halmashauri yetu kuiendesha halmashauri kimapato kutokana na wafugaji hao,” alisema.

Mbunge wa jimbo la Manyoni Mashariki, Dk Pius Chaya ameliomba Jeshi la Polisi kutoendesha operesheni zake kwenye minada kwa kutumia vitisho kwa wafugaji, badala yake wadumishe ulinzi na amani kwa ajili ya wananchi na mali zao.

Aliwataka pia wafugaji hao kutoa ushirikiano kwa wataalam wa mifugo pindi zinazotakiwa kufanyika kwa chanjo kwa ajili ya mifugo yao.

Chanzo: habarileo.co.tz