Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafugaji wadaiwa kumshambulia, kumjeruhi ofisa afya Mpwapwa

Mawe Ed Wafugaji wadaiwa kumshambulia, kumjeruhi ofisa afya Mpwapwa

Fri, 17 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ofisa Afya wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Ismail Wabu, amenusurika kifo baada ya kuvamiwa na kupigwa na watu wanaodaiwa kuwa ni jamii ya wafugaji wakati akitekeleza majukumu yake ya kuhamasisha matumizi ya vyoo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma alipolazwa ofisa huyo alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 11 alfajiri wakati wakizunguka kwenye makazi ya watu na kutoa elimu ya matumizi bora ya vyoo.

“Tulikuwa tukitoa elimu ya usafi wa mazingira na matumizi bora ya vyoo kwa wakazi wa eneo la Kikiji cha Igoji One eneo ambalo ni la jamii za wafugaji ambao wamekuwa hawatumii vyoo.

“Tulienda nyumba ya kwanza tukamkuta mama mmoja tukamchukua, tukaenda ya pili tukamkuta kijana mmoja tukamchukua na tukaenda nyumba ya tatu hatukukuta watu mara tukasikia mawe yakaanza kurushwa na wengine kupiga miluzi ndipo likatokea kundi la watu wengi wakaanza kutukimbiza” alisema.

Alisema baada ya kundi hilo kutokea walianza kukimbia na yeye kujikwaa na kuanguka ndipo walipomvamia na kuanza kumpiga kwa fimbo hadi kupoteza fahamu.

“Nilipoanguka nikawaomba msamaha wasinipige nikiwaambia kuwa sisi hatuna nia mbaya kwani tunachotaka ni kutoa elimu ya usafi wa mazingira na ujenzi wa vyoo hawakunielewa na wengine walikuwa wakisema niuawe, mmoja akanipiga fimbo ya kichwa ndipo nilipopoteza fahamu” alisema.

Alisema alipozinduka alijikuta katika vichaka huku watu wakiwa wamemzunguka ambao walimsadia kumtafutia usafiri wa pikipiki na kupelekwa katika Kituo cha Afya cha Mima.

“Nilipelekwa katika kituo hicho cha afya na kupatiwa matibabu lakini walinihamishia kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa na baadaye ikahitajika nifanyiwe kipimo cha CT scan ndipo wakanipatia rufani ya kuja hapa” alisema.

Alisema baada ya kufanyiwa kipimo hicho imebainika kuwa taya zake zote zimevunjika, hivyo anasubiri kupatiwa matibabu kulingana shida yake.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Dk. Rahim Hangai, alithibitisha kumpokea majeruhi huyo.

Alisema: “Kama ambavyo mmemuona walimpiga sana na amenusurika kifo kwani walikuwa wamuuwe ni Mungu tuu lakini hawa watu inasemekana siyo mara ya kwanza kufanya tukio kama hili nasikia hata kipindi cha nyuma walishampiga mtumishi wa halmshauri.

“Hawa ni jamii ya wafugaji ambao wao hawataki kujenga vyoo hivyo wakaamua kuwapiga wataalam wetu ambapo huyu mmoja alianguka wakati akikimbia na kumvunja taya zake na hivi sasa amelazwa katika hospitali ya rufaani ya mkoa wa Dodoma”alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live