Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafugaji kumpongeza JPM kwa maandamano

37371 Pic+maandamano Wafugaji kumpongeza JPM kwa maandamano

Sun, 20 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mashirika yasiyo ya kiserikali na viongozi wa makundi mbalimbali ya wafugaji nchini wamepanga kufanya maandamano ya amani kesho Jumamosi Januari 19, 2019 jijini Arusha, kumpongeza Rais John Magufuli kwa tamko alilolitoa kuhusu vijiji na vitongoji vinavyopakana na maeneo ya hifadhi.

Januari 15, 2019 Rais Magufuli alizuia zoezi la kuviondoa vijiji na vitongoji 366 vinavyodaiwa kuwepo katika maeneo ya hifadhi na amewataka viongozi wa wizara zote zinazohusika kukutana ili kubainisha na kuanza mchakato wa kurasimisha maeneo ya vijiji na vitongoji hivyo.

Tamko lililotolewa jana Alhamisi Januari 17, 2019 jijini Arusha kwa niaba ya wafugaji nchini na wawakilishi na taasisi mbalimbali kutoka wilaya mbalimbali za Simanjiro, Kiteto, Ngorongoro, Longido, Siha, Hannang na Monduli pia limetoa wito kwa wananchi na taasisi nyingine zilizopewa maagizo na maelekezo.

“Januari 19 mashirika na viongozi wa wafugaji nchini tumepanga kufanya maandamano ya amani kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli kama ishara ya kuonyesha kufurahishwa kwetu na maagizo na maelekezo yake kwa vyombo vya Serikali yenye nia njema na dhati ya kutetea wafugaji ambao kwa muda mrefu tumekuwa tukinyanyaswa, kufukuzwa, kuchomewa mali na kutaifishwa mali zetu katika maeneo yanayopakana na uhifadhi nchini,” lilieleza tamko hilo lililosomwa na Edward Porokwa ambaye ni mkurugenzi Jukwaa la Pingos

“Kwa hili tunadiriki kusema bila kuficha kuwa mheshimiwa Rais umetukuna wafugaji na kwamba umeonyesha dhahiri kuwa ni mtetezi wa wananchi wanyonge (wafugaji). Maandamano haya yatafanyika mjini Arusha. Tunawakaribisha wote walioguswa na tamko la Mheshimiwa Rais kuhusu wafugaji kushiriki katika maandamano haya ya amani,” ilieleza sehemu ya tamko hilo.



Chanzo: mwananchi.co.tz