Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafugaji 296 wajiandikisha kuhama Ngorongoro

Wahamiajipic Datass Wafugaji 296 wajiandikisha kuhama Ngorongoro

Wed, 15 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Zaidi ya wananchi 296 katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wamejiandikisha ili kuhama katika makazi hayo na kwenda Kijiji cha Msomera kilichopo mkoani Tanga ambapo uongozi wa Mkoa wa Arusha umesema zoezi hilo ni la hiari na utaratibu umeshawekwa.

Akizungumza na baadhi ya jamii ya kifugaji katika eneo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella amesema mpaka sasa kaya 296 zimeshajiandikisha ili kuondoka katika eneo hilo huku wananchi wengine wakitarajiwa kujiandikisha kwenda katika eneo la Msomera.

“Kule miundombinu inazidi kuimarishwa nyumba 103 ziko tayari, kesho tunaanza awamu ya kwanza ya kupeleka mifugo, mali zao pamoja na wao wenyewe kwani tumeshajitayarisha,” amesema Mongella

Baadhi ya wananchi ambao wapo tayari kuondoka kwa hiari katika eneo hilo wamesema wameridhia kuondoka katika maeneo hayo kwani wanafidiwa kila kitu ikiwamo kujengewa nyumba na huduma mbalimbali ambazo Rais (Samia Suluhu Hassan) anawapa.

“Unapewa fidia kwa halali yako bado unapewa na nyumba bado Rais Samia analeta zawadi yake kwetu kama mama. Hatujawahi kuona watu wakifanyiwa hivyo kama sisi wana- Ngorongoro,” amesema Danieli Huho.

Wameongeza kuwa fursa hiyo waliyopewa ni bahati na upendeleo kwa wana-Ngorongoro kwani licha ya kupewa nyumba, mashamba na huduma nyingine lakini wamewezeshwa ili kuweza kuendana na kasi ya maendeleo.

“Kuna shule, hospitali nzuri, miundombinu ya maji vikiwepo visima ambapo katika mzunguko wa nyumba kuna ekari 3 mbali na mashamba yenye ekari 5. Pia Rais Samia ametuwezesha ili tukitoka hapa tukaendane na kasi na kubadilisha maisha kwa kuwa hapa tumepoteza muda, tungeletewa hii fursa mapema tungekuwa mbali zaidi,” amesema Beatrice Soka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live