Mbeya. Watu wawili wamekufa baada ya kutumbukia mtoni wakati wakipita katika daraja linalounganisha kata ya Tembela na Mwakakibete mjini Mbeya.
Akizungumza leo Jumatatu Oktoba 7, 2019 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na kusema kuwa jitihada za kutafuta miili mingine zinaendelea.
Diwani wa Tembela, Anderson Ngao amesema watu wanne walisombwa na maji baada ya daraja hilo kuvunjika wakati wakipita, wawili hawajulikani walipo, akiwemo wa umri wa mwaka mmoja.
"Mtu mmoja aliyenusurika ndio shahidi wetu kwamba walisombwa na maji watu wanne, maiti moja tuliipata jana na nyingine tumeipata leo asubuhi," amesema.
Ofisa mtendaji kata ya Tembela, Lington Mfwango amesema daraja hilo limevunjika kwa mara ya pili na kwamba mara ya kwanza halikuleta madhara.