Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyakazi wanaojenga bandari Dar wagoma

47295 Pic+wafanyakazi

Tue, 19 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi ya China (Chec), wamegoma kufanya kazi wakishinikiza iwapatie mikataba yenye masilahi bora ikiwamo nyongeza ya mishahara na marupurupu mengine.

Mgomo huo umehusisha wafanyakazi wa kada mbalimbali ambao kwa pamoja wanalalamikia matatizo yanayofanana.

Wameilalamikia kampuni ya Vipaji Link ambayo inashughulikia rasilimali watu katika kampuni ya Chec kwamba inawahujumu.

Akizungumzia mgomo huo leo, Jumatatu, Machi 18, 2019 mjumbe wa chama cha wafanyakazi wa kampuni hiyo kiitwacho Tasiw, Suleiman Omary amesema hawautaki mkataba wa zamani kwa sababu hauna masilahi kwao na kwamba mwajiri wao amekuwa haufuati.

“Kwa kifupi sisi tunataka mkataba wenye hali bora ambao utakuwa na mambo manne ambayo ni mshahara mzuri wa mfanyakazi, hela ya chakula, hela ya matibabu na usafiri,” amesema Omary.

Pia amesema wanataka pia kampuni ya Vipaji Link iondoke kwa sababu wamekuwa wakifanya kazi kama madalali kati ya Wachina na wafanyakazi, jambo ambalo wanadai linadumaza masilahi yao.

Kwa upande wake, Masoud Nassoro, kampuni hiyo alisema kuna wafanyakazi kutoka China ambao wanafanya kazi ambazo kisheria zinatakiwa kufanywa na Watanzania.

Amesema wapo wanaoendesha katapila, wapishi na wanaofanya usafi.

“Mbali na kukandamiza masilahi yetu, wapo pia Wachina wanaofanya kazi za kawaida ambazo zinatakiwa zifanywe na Watanzania. Tunaiomba Serikali itembelee hapa kuona jinsi kulivyo na ukiukwaji wa sheria,” amesema.

Viongozi wa kampuni hiyo hawakutaka kuzungumzia kuhusu suala hilo na kuagiza walinzi wao kutoruhusu waandishi wa habari kuingia ofisini.

Hata hivyo, viongozi wa wafanyakazi wamekuwa kwenye mazungumzo na uongozi wa kampuni hiyo.



Chanzo: mwananchi.co.tz