Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyakazi waandamana kudai mishahara, michango ya NSSF

Waandaana Mgodi.png Wafanyakazi waandamana kudai mishahara, michango ya NSSF

Tue, 12 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Baadhi ya wafanyakazi wa mgodi wa dhahabu wa Cata uliopo Kijiji cha Kataryo Wilaya ya Butiama mkoani Mara wameandamana wakiutaka uongozi wa mgodi huo kuwalipa madai yao ikiwemo mishahara.

Wafanyakazi hao ambao ni sehemu ya wafanyakzia 342 wa mgodi huo, waliandamana Septemba 11, 2023 hadi katika geti kuu la kuingila mgodini humo kisha kupokelewa na Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwandani na Taasisi za Fedha (Tuico) Mkoa wa Mara.

Wakizungumzia maandamano hayo, wafanyakazi hao wamesema madai yao ni pamoja na mishahara ya miezi miwili iliyopita hali ambayo imepelekea hivi sasa kuishi maisha magumu.

“Hatujapokea mshahara wa mwezi Julai na Agosti na dalili zinaonyesha hata huu mwezi Septemba pia hakuna mshahara,”amesema Reuben Omollo

Amesema mbali na mishahra lakini pia wafanyakzi hao wamebaini kuwa michango yao haipelekwi kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii (NSSF) kwa mujibu wa sheria jambo ambalo ni hatari kwao hasa watakapokuwa wamestaafu.

Mfanyakazi mwingine, Jackson Amulike amesema walikutana na uongozi wa mgodi huo chini ya Ofisa madini wa Mkoa ambapo uongozi huo uliahidi kulipa mishahara ya miezi miwili ifikapo Septemba 7 mwaka huu ahadi ambayo haijatimizwa hadi sasa.

“Badala ya kutulipa kama tulivyokubaliana wametoa tena memo eti malipo sasa yatafanyika Septemba 19 hii haikubaliki,"amesema Amulike

Amesema hali hiyo imesababisha wafanyakazi hao kuishi maisha magumu kutokana na kutokuwa na fedha za kujikimu huku wengine wakilazimika kuyakimbia makazi yao kwa kukosa pesa za kulipa kodi.

“Watu tumepanga tunategemea mishahara ili tuweze kulipa kodi kuna wenzetu ambao wenye nyumba wameshindwa kuwaelewa imebidi wayakimbie makazi yao na kujibana kwa wenzao maana hawana namna yoyote ile ya kufanya,"amefafanua

Kufuatia hali hiyo wafanyakazi hao wameiomba Serikali kuingilia kati ili waweze kulipwa stahiki zao.

Boniphace Maxmillian amesema mbali na mishahara, wafanyakazi hao wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu ambapo wanalazimika kununua vifaa vya usalama kazini (safety gears) badala ya kununuliwa na mwajiri kwa mujibu wa taratibu.

“Lakini kampuni hii imekuwa na utaratibu wa kutozingatia maslahi ya wafanyakazi wake mfano kuna kipindi mgodi ulifungwa tangu Mwaka 2017 hadi 2019 lakini hadi sasa waliokuwa wafanya kazi katika kipindi hicho hawajalipwa madai yao,"amesema

Amesema pia kampuni haina utaratibu wa kulipia huduma za afya, likizo za mwaka, kodi za nyumba pamoja na nyongeza ya mishahara kwa wafanyakazi kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria na taratibu.

Ofisa Madini Mkoa wa Mara, Amini Msuya amekiri kupokea malalamiko ya wafanyakazi hao na kwamba tayari wameiagiza kampuni kuyashughulikia.

“Tulikutana na uongozi wa kampuni, wafanyakazi na NSSF uongozi ukaahidi kulipa mishahara ifikapo Septemba 7 pia kupeleka michango NSSF kama inavyotakiwa lakini tumepoeka tena barua kutoka mgodini ambayo inasema sasa mishahara hiyo italipwa Septemba 19,"amesema Msuya

Amefafanua kuwa baada ya kufuatilia kwa ukaribu sababu ya kuchelewa kwa malipo hayo walibaini kushuka kwa uzalishaji hali ambayo kwa namna moja imechangia kampuni kushindwa kulipa mishahara kwa wakati lakini uongozi umeahidi kutafutia ufumbuzi suala hilo.

Mkuu wa Idara ya Utawala na Fedha wa Cata, George Msekalile amekiri wafanyakzi hao kudai mishahara ya miezi miwili sasa na kwamba hali hiyo imetokana na uzalishaji wa kampuni kushuka.

"Matumizi yetu kwa mwezi ni zaidi ya Sh3.8 bilioni wakati tunazalisha Sh1.9 bilioni sasa unaweza kuona namna gani uzalishaji unaathiri matumizi kwasababu matumizi yetu yako pale pale haijalishi uzalishaji umeshuka au kupanda,"amesema Msekalile

Amesema uongozi unafanya jitihada ili kuboresha uzalishaji ili kuweza kwenda sambamba na mahitaji ikiwemo kulipa mishahara ya wafanyakazi.

"Tuna mipango mingi ili kuimarisha na kuongeza uzalishaji, mipango hiyo ni pamoja na kuanza uchimbaji wa underground na tunaamini mambo yatakuwa sawa," amesema

Chanzo: www.tanzaniaweb.live