Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyakazi wa ndani wapewa mikataba, elimu ya kujikomboa

15476 Pic+wafanyakazi TanzaniaWeb

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ukosefu wa mikataba ya kazi kwa wafanyakazi wa nyumbani umetajwa kuwa sababu mojawapo ya baadhi ya wafanyakazi hao kutenda vitendo vya kikatili ikiwemo kuwapiga na kuwanyanyasa watoto wa waajiri wao na wakati mwingine kutojali suala zima la mlo wa watoto hao.

Tatizo hilo pia linatajwa kwa mojawapo ya sababu za waajiri wengi kuwafanyia vitendo vya aibu wafanyakazi wao ikiwemo kuwapiga, kuwanyanyasa kijinsia ikiwamo kuwabaka na mateso mengine ya kisaikolojia.

Changamoto hiyo imeliibua shirika la kutetea haki za wafanyakazi wa nyumbani la Wotesawa lililopo jijini Mwanza kuja na mkakati wa kuhakikisha mwajiri anampatia mkataba wa kazi mfanyakazi wake utakaomlinda kwa mambo mengi ikiwamo vitendo hivyo vya kikatili na visivyokubalika.

Mratibu wa mradi wa ujengewaji uwezo wa kijamii na kiuchumi kwa mtoto na kijana kutoka shirika la Wotesawa, Elisha David anasema kwamba kupitia mradi huo wameweza kusaidia wafanyakazi 36 kati ya waajiri 87 waliopatiwa elimu ya umuhimu wa kuwapatia mikataba ya kazi tangu walipoanzisha kampeni hiyo mwaka 2017.

David anasema kwamba mikataba hiyo itapunguza vitendo vya kikatili walivyokuwa wanafanyiwa wafanyakazi hao ikiwemo vile vya kingono, kiuchumi na kufanyishwa kazi bila malipo ama kwa malipo kidogo na ambayo wakati mwingine hayaendani na kile wanachokifanya.

Anasema hali hiyo itawasaidia wafanyakazi hao kuweka fedha zao ili zije ziwasaidie katika kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo kuanzisha, miradi na wengine kurudi shule kujiendeleza na hivyo kupunguza taifa la watu wasiojua kusoma na kuandika lakini pia kukuza uchumi.

Tafiti zilizofanywa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2014 zilibaini kuwepo wafanyakazi wa ndani milioni 15.5 kati ya hao asilimia 75 ni vijana wenye umri kati ya miaka 10 na 18.

Halikadhalika takwimu zilizotolewa na shirika lisilo la kisekali la Wotesawa la jijini Mwanza linalofadhiliwa na The foundation for Civil Society katika kata sita za Igogo, Mkuyuni, Mkolani, Buhongwa, Butimba na Nyamagana zilibaini watoto 438 wameajiriwa kufanya shughuli mbalimbali za nyumbani.

David anasema kwamba kati ya wafanyakazi hao asilimia 40 wanafanya kazi zinazowatesa huku asilimia 60 hawajaenda shule na kwamba hakuna uwepo wa sheria, kanuni wala mikakati ya kumlinda mfanyakazi wa nyumbani.

“Tuliamua kubuni mradi wa kuhamasisha jamii na viongozi wa serikalini kuhakikisha wanakomesha vitendo vya kikatili lakini pia kuhakikisha wanawatambua wafanyakazi wa ndani na kuwasaidia kupewa mikataba,” anasema David.

David pia anasema kwamba shirika hilo lilianzisha vikundi vya wafanyakazi wa nyumbani ambapo hadi sasa vipo sita na vimesajiliwa kisheria ili vianze kunufaika na asilimia nne ya mapato ya ndani ya halmashauri ambayo yanatakiwa kutolewa kwa vijana.

“Lengo ni kupunguza mifumo yote ya ukatili na unyonyaji kwa mfanyakazi, kufanya masuala ya utetezi, pamoja na kuwajengea uwezo kuhusu afya ya uzazi ili waweze kujisimamia wao wenyewe,”anasema.

Moja ya matukio ya kikatili ya kukumbukwa ni lile la mfanyakazi wa ndani mtaa wa Msikitini kata ya Mkuyuni, kushambuliwa kwa kupigwa na mwajiri wake kwa kosa la kuvunja glasi ya kunywea maji.

Mbali na kipigo hicho pia mwajiri huyo alimchomea nguo zake na kumtembeza mtaani akiwa mtupu kitendo kilicholaaniwa na aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Nyamgana, Merry Tesha ambaye pia aliwataka viongozi wa kata hiyo kumchukulia hatua mwajiri huyo.

Kwa upande wake, ofisa utetezi wa Shirika la Wotesawa, Veronica Rodrick anasema kwamba waajiri wengi wanadaiwa kukiuka sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009, sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2017, waraka wa mishahara wa mwaka 2013 pamoja na katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Anasema wapo waajiri tena wengi tu ambao wanaajiri na hawawalipi mishahara kama inavyotakiwa na wala hawako tayari kuwapa wafanyakazi wao nafasi ya kujiendeleza kimasomo, kujishughulisha na ujasiriamali au masomo ya ufundi na kuwapa muda wa kupumzika.

Zaidi ya hilo anaongeza kuwa wafanyakazi pia wanabaguliwa, kutengwa na pia kutopatiwa huduma nyingine mhimu ikiwamo kutibiwa anapoumwa.

Kuhusu suala la mshahara anasema waajiri bado hawawalipi kiwango kamili cha Sh40,000 kilichopendekezwa na Serikali kwa mfanyakazi anayeishi nyumbani na Sh80,000 kwa yule anayeishi nje ya nyumba.

“Mfanyakazi huyo pia imebainika kuwa wakati mwingine hapatiwi hata muda wa kupumzika kama mfanyakazi mwingine au kupewa likizo ya kila mwaka ili kumsaidia kujiepusha na vitendo vya kikatili anavyoweza kufanya,”anasema Veronica.

Viongozi wanasemaje?

Mkuu wa kitengo cha dawati la jinsia na watoto mkoani Mwanza, Bethnsimbo Shija anasema kwamba mfanyakazi wa nyumbani anaweza kusababisha athari za kimazingira kwa sababu hapewi uhuru na muda wa kupumzika.

Mwenyekiti wa mtaa wa Nyamalango, Ndaki Godi anasema kwamba kabla hawajapata elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa wafanyakazi wa ndani kulikuwa na matukio mengi ya namna hiyo kwenye mtaa wake.

Anasema kwamba mtaa huo unaozungukwa na taasisi tatu za elimu zinaajiri watumishi wengi ambao hapo awali walikuwa hawawalipi wafanyakazi wao mshahara kama inavyokusudiwa.

“Baada ya kupata elimu, tuliweza kubaini uwapo wa wafanyakazi wa ndani 38 wanaofanyakazi mbalimbali zikiwemo za kulisha mifugo na nyingine za ndani,” anasema Godi

Mwenyekiti huyo alipongeza shirika la Wotesawa kwa kuwapatia elimu hiyo ambayo anasema imewajengea uwezo wa kutatua migogoro inayotokea baina ya mwajiri na mfanyakazi lakini pia kuendelea kuhamasisha jamii kujua umuhimu wa kuwapatia mkataba wafanyakazi wao.

“Kupitia elimu hiyo, mimi na wazee wa mtaa imetusaidia kutatua migogoro 19 ya wafanyakazi wa ndani ambao walikuwa wananyanyaswa na waajiri wao lakini pia hawalipwi mishahara yao kikamilifu,” anasema Godi

Mwenyekiti huyo pia anabainisha changamoto wanazokutana nazo baadhi ya wafanyakazi wanaotoroka nyumbani kwao kuja kutafuta kazi maeneo ya mjini na wakati huo hawana mawasiliano na wazazi wao.

Wafanyakazi wa ndani wanasemaje?

Mfanyakazi wa ndani mtaa wa Mkuyuni, Adella Alikadi anasema kwamba kabla hawajapata elimu kutoka Shirika la Wotesawa baadhi yao walikuwa hawalipwi mishahara yao na wakati mwingine walikuwa wanapewa zawadi au kiasi kidogo cha fedha.

Adela ambaye ni kati ya wafanyakazi 50 waliopatiwa elimu anasema hawakujua haki zao na waliponyanyaswa hawakuwa na sehemu ya kwenda kutoa taarifa.

“Sasa hivi nina mkataba na ninalipwa fedha zangu zote kwa mujibu wa sheria na ninatunza fedha hizi ili zinisaidie kuanzisha mradi kwa kuwa napenda kuwa mjasiriamali,” anasema Adella.

Mfanyakazi mwingine, Tatu Ally anasema pamoja na kupatiwa mikataba hiyo lakini wanatamani kuwa sehemu ya familia.

Tatu ambaye anajifunza ufundi cherehani analishukru Shirika la Wotesawa kwani kupitia elimu waliyopata kutoka kwao na mwajiri wake imemsaidia kupewa mshahara wake wote uliomsaidia kununua cherehani ambayo ni mtaji wa kuendesha shughuli za ushonaji.

Mwajiri anasemaje?

Mkazi wa Nyegezi jijini Mwanza, Johari Mussa anasema kwamba hapo awali hawakujua umuhimu wa kuwapatia mikataba wafanyakazi wao na waliona kuwa hilo ni jambo la kawaida kwa kuwa walikuwa kwenye sekta ya ajira isiyorasmi.

“Sasa tunalazimika kuwapatia mikataba na kwamba wameanza kufanya hivyo baada ya kupata elimu kutoka Shirika la Wotesawa,” anasema Johari.

Johari anawataka waajiri wengine kuhakikisha wanawapatia wafanyakazi wao mikataba kwani hiyo inawasaidia na kuwapa moyo wa kufanya kazi lakini pia kupunguza migogoro na migongano iliyokuwa inatokea huko nyuma.

Chanzo: mwananchi.co.tz