Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyakazi Mtwara wafurahia elimu ya sheria za kazi

22022 Korosho+pic TanzaniaWeb

Fri, 12 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara. Zaidi ya wafanyakazi 300 wa kiwanda cha kubangua korosho cha Micronix kilichopo mkoani Mtwara wamefurahia kupewa elimu ya sheria za kazi mahali pa kazi kutokana na kutokuwa na elimu hiyo hapo kabla.

Wakizungumza leo Alhamisi, Oktoba 11 baada ya kutembelewa na maofisa wa kazi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, wafanyakazi hao wamesema wamekuwa hawazitambui haki zao na hivyo kushindwa kufanya kazi kwa ustadi.

Mmoja wa wafanyakazi hao, Ritha Minja amesema elimu hiyo itawasaidia wanapopata matatizo sehemu za kazi wajue ni waende wapi.

“Ninaona ujio wa watu wa wizara ya kazi ni wa muhimu sana kwa sababu wengi tunashindwa kufanya kazi kwa ustadi na faida kwa sababu hatujui sheria na haki zetu ambazo ni suala la msingi sana, mimi kama mfanyakazi sijui wajibu wangu katika kazi, na mwajiri akiwa hajui wajibu wake wa kumpatia mfanyakazi hilo ni tatizo,”amesema Minja.

Naye Frank Tayari amesema kabla ya elimu hiyo wamekuwa wakifanya kila anachotakiwa na mwajiri wao lakini sasa endapo haki zao zitakiukwa watakuwa wanaelewa.

“Siku za nyuma kila tulichoambiwa tulikuwa tunafanya lakini leo tumepata elimu tumefahamu wajibu wetu ni nini na haki zetu ni zipi mfano wakati wa kuingia kazini au ufanyaji kazi siku za sikukuu,” amesema Tayari.

Ofisa kazi kutoka wizara hiyo, Suleiman Seng’ege amesema wafanyakazi wanapokuwa na uelewa juu ya sheria za kazi watafanya kazi wakiwa na amani na ari na eneo la kazi litakuwa na amani.

“Hakuna kitu kizuri kama ukiwa unafanya kazi ukitambua wajibu wako ni upi na haki yako ni ipi, mwisho wa siku tija itakuwepo na mkileta tija familia zenu na Taifa litanufaika, serikali inachokifanya ni kuhakikisha pande zote mbili zinatimiza matakwa ya sheria za kazi na hapo ndipo amani maeneo ya kazi itapatikana na kila upande utanufaika,” amesema Seng’ege

Meneja wa tawi la kiwanda hicho, Sivan Edayadath amesema wamekuwa wakiendesha kiwanda hicho kwa kufuata sheria zote lakini elimu ambayo wamepatiwa itasaidia kuboresha ufanisi wa kazi zaidi.

Kiwanda hicho kimeajiri wanawake 320 na wanaume 19.

Chanzo: mwananchi.co.tz