Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara wa nyama wagoma Mwanza

43764 Pic+nyama Wafanyabiashara wa nyama wagoma Mwanza

Tue, 26 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Wafanyabiashara wa nyama jijini Mwanza wamegoma kuchinja ng’ombe kwa muda usiojulikana.

Wakizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Februari 25,2019, wafanyabiashara hao wamesema wamegoma kufanya shughuli hiyo kwa sababu ya gharama kubwa za ushuru na kusafirishia ng’ombe kutoka wilayani Misungwi hadi jijini Mwanza inayofikia Sh33,300.

Dominick Edwald mfanyabiashara wa nyama wa Soko Kuu jijini humo, amesema wanapata hasara kwa sababu mnada wa ng’ombe upo mbali hali inayosababisha ng’ombe kufia kwenye magari.

“Serikali ituangalie wajasiriamali, watusogezee mnada huko ulipo mbali na gharama za usafirishaji ni kubwa,” amesema Edward.

Hata hivyo, wafanyabiashara hao wamekubaliana kuuza nyama ya mbuzi kwa kuwa hawana gharama, mbuzi mmoja anagharimu Sh8,000 kutoka machinjioni hadi kwenye maduka ya nyama.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Soko Kuu, Hamad Nchola amesema amepewa mchanganuo wa gharama zilizosababisha wafanyabiashara hao wagome ni wanaponunua ng’ombe wilayani Misungwi wanatozwa Sh6,500 za ushuru na kusafirisha kwa Sh6,000.

Amesema kupakia ng’ombe mmoja kutoka Misungwi hadi Igoma machinjioni ni Sh1,000, malipo ya machinjioni ni Sh9,000, mchinjaji hulipwa Sh600, usafirishaji kutoka machinjioni hadi kwenye mabucha Sh5,000 nauli ya mtu anayeenda na kurudi Misungwi Sh4,200 na upakiaji wa nyama kwenye magari ni Sh1,000.

“Nilivyopiga mahesabu hayo nikaona ng’ombe mmoja anagharamikia Sh33,300 na wenyewe wakasema hawapati faida wanapata hasara tu, kama kiongozi nikawaambia kwa nini wasikae na uongozi wa wilayani Misungwi na jijini Mwanza kwa kuwa ni Wilaya mbili tofauti ili wapunguze kwa sababu haiwezekani ng’ombe mmoja awe na gharama kama hiyo,” amesema Nchola.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz