Songea. Wafanyabiashara mkoani Ruvuma wametaja kero zao mbalimbali zinazosababisha washindwe kufanya biashara kama inavyotakiwa, kuiomba Serikali ya Tanzania kuzifanyia kazi.
Wameeleza hayo leo Jumanne Septemba 24, 2019 katika mkutano kati yao na mawaziri mbalimbali waliokuwa wakisiliza kero na changamoto zao.
Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Jumuiya ya Wafanyabiashara na Wajasiriamali wadogo ndio waliowasilisha kero hizo katika mkutano huo uliofanyika mjini Songea mkoani Ruvuma.
Mawaziri walioshiriki mkutano huo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki; naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Musa Sima; naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angela Mabula na naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji.
Katibu wa jumuiya ya wafanyabiashara mkoani Ruvuma, Wilson Nziku amesema ubovu wa miundombinu inayounganisha Mkoa huo na nchi jirani ya Msumbiji na Malawi, utitiri wa kodi, ucheleweshaji wa malipo na Serikali kutosimamia vyema sekta ya kilimo hasa usambazaji wa pembejeo na usimamizi wa mifumo ya masoko ya mazao ni kati ya kero hizo.
Alizitaja kero nyingine kuwa ni wakulima kutozwa ushuru kabla ya mazao kufika sokoni na kampuni kubwa kutokuwa na mfumo mzuri wa usambazaji wa pembejeo kwa kutofautisha bei ya jumla na rejareja.
Pia Soma
- Washtakiwa uhujumu uchumi waanza kuomba msamaha
- Moto wateketeza wodi ya wazazi, waua vichanga wanane
- Waziri Mkuu Uingereza apata pigo jingine
“Pia gharama kubwa ya maeneo ya biashara yanayomilikiwa na manispaa mfano miji mingine vibanda vya biashara vinavyokodishwa kwa 150,000 kwa mwezi Ruvuma ni kati ya Sh250,000 hadi 400,000 kwa mwezi,” amesema Nziku.
Nziku amezitaja baadhi ya kodi zikiwemo za zuio katika maeneo ya biashara, zimamoto, mabango ya biashara kuwa vikwazo, “Yaani unapaswa kuwa na leseni zaidi ya moja katika duka eti kwa kuwa unauza bidhaa mchanganyiko.”
Mwakilishi wa sekta ya viwanda, Alex Tweve amezitaja changamoto kadhaa za biashara ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoza kodi kubwa na riba pamoja na mamlaka mbalimbali za kutoa vibali vya biashara kutokuwa na ofisi mkoani humo.
Tweve amezitaja taasisi hizo ambazo hazina ofisi kuwa ni Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha), NEMC na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA).
Akijibu baadhi ya kero, Dk Kijaji alisema katika bajeti ya 2018/19 na 2019/20, Serikali ilitenga Sh600 bilioni kwa ajili ya kulipa madeni ya wazabuni na watumishi na mkoa huo ulipewa Sh500 milioni.
Mbali na kuwataka wafanyabiashara kuwa waaminifu kwa kulipa kodi, Dk Kijaji amesema Serikali imefuta tozo 54 zilizokuwa kero kwa wafanyabiashara na wawekezaji, bado inaendelea kuziondoa na kuzifanyia marekebisho ili kuweka mazingira sawa ya biashara.
Kwa upande wake Kairuki amesema Serikali imedhamiria kukuza mchango wa viwanda hasa vya mazao ya kilimo jambo litakalokuza ajira kwa wananchi wa vijijini.