Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara Ruksa Soko la Karume

Machinga Pic Data Wafanyabiashara wa Soko la Karume, Ilala

Mon, 17 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wafanyabiashara wa soko la Karume (Mchikichini) wameruhusiwa kuweka alama kwenye maeneo yao ili wajihakikishie usalama wakati wakisubiria ripoti ya kamati iliyoundwa kuchunguza chanzo cha moto uliosababisha kuteketea kwa soko hilo.

Uamuzi huo umefikiwa leo Jumatatu Januari 17, 2022 kwenye kikao kilichofanyika kati ya viongozi wanaowawakilisha wafanyabishara hao na Mkuu wa Wilaya ya Ilala (DC), Ng'wilabuzu Ludigija baada ya maandamano yaliyofaywa kushikiza waruhusiwe kuingia kwenye eneo hilo kuendelea na shughuli zao.

Mapema leo wafanyabiashara hao waliandamana mpaka kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla kushinikiza kiongozi huyo atoe tamko la kuwaruhusu waendelee kufanya shughuli zao kwenye soko hilo.

Katika maandamano hayo walifunga barabara kwa kutumia magogo na mawe katika makutano ya barabara ya Uhuru na Kawawa Ilala Boma huku Polisi wakilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.

Hali hiyo ilisababisha kufanyika kikao kati ya viongozi wanaowawakilisha wafanyabishara hao na DC Ludigija ambapo kikao hiccho kilifikia uamuzi wa kuwaruhusu kuweka alama maeneo yao.

Akizungumza baada ya kikao hicho Msemaji wa wafanyabishara hao, Ismail Feisal amesema katika kikao hicho wamekubaliana na Serikali kuanzia leo shughuli ya kuweka alama hizo ianze.

Tunashukuru tumekubaliana na Serikali kwamba tuweke alama wakati kamati ikiendelea kuchunguza kubaini chanzo, unajua mwanzo tulifanya maandamano ya amani tulikosa imani na maagizo yao baada ya kupata taarifa Serikali inataka kukodisha eneo hili kwa muwekezaji tuliona haki yetu inaweza kupoteza," amesema Feisal

Feisal amewatuliza wafanyabishara wenzake na kuwataka kuondoka kwenye ofisi hizo za mkuu wa mkoa kuelekea kwenye eneo lilikoteketea soko ili kila mmoja ajihakikishie eneo lake likiwa salama bila kuingiliwa na mtu.

Mkuu wa Wilaya amewaahidi kuwa baada ya siku saba zilizotolewa na Serikali kufanya uchunguzi zikipita, wafanyabishara hao wataruhusiwa kuanza kujenga mabanda yao na kuendelea na shughuli zao.

"Tunafanya hivi kwa kuacha uchunguzi ufanyike ili kubaini chanzo na hatua zichukuliwe nasi kuacha wa sababu soko hili limeungua kwa mara tatu sasa hatuwezi kuacha watu waendelee kupata hasara,"amesema

Amesema ofisa Masoko wa Jiji, mtendaji wa kata ya Mchikichini na viongozi wa wafanyabishara hao watasimamia uwekaji wa alama.

Jana Jumapili baada ya soko hilo kuungua Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Amos Makalla aliagiza wafanyabiashara hao kusitisha shughuli zote katika eneo hilo mpaka kamati ya uchunguzi itakapokamilisha kuchunguza

Chanzo: www.tanzaniaweb.live