Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wafanyabiashara Kibaha walia ubovu wa soko

Wafanyaboiashara Kibaha Wafanyabiashara Kibaha walia ubovu wa soko

Sat, 23 Dec 2023 Chanzo: Mwananchi

Wafanyabaishara wa Soko la Mnarani maarufu kwa jina la Loliondo katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani wamewataka viongozi wapya waliowachagua, kuhakikisha wanaanza na kero ya uchakavu wa soko hilo.

Wametoa kauli hiyo jana usiku Desemba 22, baada ya kukamilika kwa uchaguzi uliohusisha uongozi wa soko hilo ambao watahudumu kwa kipindi cha miaka mitatu.

"Tunashukuru uchaguzi umepita wapo waliorudi na wengine wapya tunachowaomba waanze na changamoto ya kukarabati paa la jengo upande wa matunda, haliko vizuri kuna maeneo kuna vuja kiujumla haliko vizuri," amesema mfanyabiashara Mbwana Shekarage.

Mfanyabiashara mwingine, Aisha Selemani amesema kuchakaa kwa paa hilo la matunda kunawapa kero kubwa iwe mvua iwe jua na pia halipitishi hewa na mvua zikianza kunyesha linavuja.

"Matunda hayatakiwi kupikwa lakini yanapikwa na joto na tunapata hasara kwa kuwa yanaoza kwa muda mfupi," amesema Aisha.

Mohamed Omary aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti wa soko hilo, amesema lengo lao ni kushughulikia kero za wafanyabiashara wenzao.

"Naelewa changamoto zilizopo ambazo hata mimi ninaziishi kubwa zaidi ni pamoja na hilo suala la paa la jengo la matunda, mimi na wenzangu tutakaa na uongozi wa halmashauri ili tuangalie tunaanzaje na naamini litafanyiwa kazi," amesema Omary ambaye amechaguliwa kwa mara ya pili baada ya kumshinda mpinzani wake Levis Maganga kwa kupata kura (485) na mwenzake kura (132).

Sifa Nguba aliyechaguliwa kwa nafasi ya katibu wa kitengo cha fremu amesema kazi yake ya kwanza katika utekelezaji wa majukumu yake ni kuhakikisha fremu zilizowazi zinapata wapangaji ili kukuza mapato ya tozo.

"Ni mgeni kwenye nafasi hii lakini naahidi kuwa karibu na viongozi wenzangu ili tufanye kazi inayoonekana na kuleta manufaa si tu kwa wafanyabishara pekee bali hata halmashauri yetu," amesema Nguba.

Msimamizi wa uchaguzi huo kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Iddi Hassan amewataka viongozi hao kujali thamani waliyopewa na waliochini yao.

Akizungumia kero hiyo kwa njia ya simu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani Mussa Ndomba amesema wana mpango wa kukarabati soko zima Ili kuwezesha wafanyabiashara kuendesha shughuli zao kwa uhakika.

"Mwishoni mwà mwaka tulitenga bajeti ya Sh40 milioni kwa ajili ya ukarabati mdogo hata hivyo pesa hiyo haijaingizwa kwenye mfumo kutokana na hatua mbalimbali lakini kwenye baraza la juzi madiwani tuliazimia kuwa mwakani tuanze na ukarabati wa soko zima," amesema Ndomba.

Chanzo: Mwananchi