Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waendesha bodaboda, DC Tanga wavutana

Thu, 9 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga. Sakata la waendesha bodaboda Jiji la Tanga kugoma kununua vitambulisho vya wafanyabiashara ndogo kwa maelezo kuwa haviwahusu, limechukua sura mpya baada ya mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa kusema kuna jambo litafanyika ikiwa wataendelea na msimamo wao huo.

 

Mvutano kati ya mkuu huyo wa wilaya na madereva hao ni baada ya Mwilapwa kusema kuanzia Mei 5, 2019 kila dereva wa bodaboda anapaswa kuwa na kitambulisho hicho.

 

Wakizungumza na Mwananchi Digital, leo, Alhamisi, Mei 9, 2019, madereva hao wamesema hawakubaliani na kauli ya mkuu huyo wa wilaya.

 

“Hatuelewi kwa nini tunalazimishwa kununua vitambulisho kwa sababu kwanza ni hiari, pili Waziri Mkuu alishaagiza kwamba ma-DC wasilazimishe na tatu sisi tuna TIN namba," amesema Jumanne Julius, mmoja wa madereva hao.

 

Amesema wao ni wafanyabiashara rasmi ambao wanalipa tozo mbalimbali TRA na wanatambuliwa na Serikali, ndiyo maana wametengewa vituo tofauti na wamachinga ambao hawana vituo maalumu na ni vigumu kuwapata.

 

Kwa upande wake, Mwilapwa amesema alishakutana na madereva hao mara nne kuwaelimisha kuhusu uhalali wao wa kununua vitambulisho hivyo na walishakubaliana kwamba watanunua.

 

“TIN namba wanazosema ni za pikipiki wanazoendesha ambazo kimsingi zinakatwa na mmiliki wa chombo hicho, lakini madereva wengi siyo wamiliki na licha ya kuwa na TIN namba, lakini hawana leseni za biashara hiyo kama ilivyo kwa wafanyabiashara wengine,” amesema Mwilapwa.

 

Amesema sababu nyingine ya kuwahimiza wanunue vitambulisho hivyo ni kwamba, biashara wanayofanya haizidi pato ghafi la Sh4milioni kwa mwaka, na ili wasibughudhiwe ni vyema wakawa na vitambulisho hivyo.

“Hoja yangu inasimamia sehemu mbili, ya kwanza ni sheria ya fedha ya mwaka 2017 iliyopitishwa na Bunge inayompa mamlaka kamishna wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) kusajili na kuwatambua wanaofanya biashara, na pili ni kauli ya kiongozi wa nchi ambaye kwa huruma yake ametusaidia sisi wasaidizi wake kwa kuchapisha vitambulisho vyenye hadhi.”

Katika awamu ya pili ya ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara ndogo, Wilaya ya Tanga ilipewa vitambulisho 7,500 ambapo hadi kufikia April 30, 2019  vitambulisho 4,008 vilikuwa vimeshanunuliwa huku Mkoa wa Tanga ukiwa umefikia asilimia 72 ya kuvigawa kwa wajasiliamali.



Chanzo: mwananchi.co.tz