Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waeleza umuhimu wa elimu jumuishi kwa walemavu

8d99263db28cd994b2d5c94c7faeaa10.jpeg Waeleza umuhimu wa elimu jumuishi kwa walemavu

Thu, 26 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

ELIMU jumuishi ni suluhisho kwa watu wenye ulemavu badala ya elimu maalumu ambayo inawatenga na kuwafanya wawe wapweke, imeelezwa.

Akizungumza wakati wa mafunzo kwa walimu wadhibiti wa elimu kutoka katika Wilaya ya Bahi na Dodoma Mjini, mwezeshaji Fortunatus Jumbe alisema elimu jumuishi ni msaada mkubwa kwa watoto wenye ulemavu.

Katika utoaji wa elimu hiyo, Jumbe alisema wameamua kwanza kuwajengea uwezo wa kitaaluma ya watu wenye ulemavu walimu ambao wana dhamana ya kusimamia na kudhibiti ubora shuleni ili wawe chachu ya kushawishi na kutetea watoto wenye ulemavu kupata elimu pamoja na wanafunzi wengine.

Alisema kwa kuwapa mafunzo kuhusu umuhimu wa elimu jumuishi wadhibiti wa ubora wa elimu kutasaidia kutia hamasa na kuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii na wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuwapeleka shuleni, badala ya mila na desturi potofu za kuwafungia ndani.

Mratibu wa elimu jumuishi katika wilaya ya Dodoma Mjini na Bahi, Jane Mdigande alisema baada ya mafunzo hayo kwa walimu wadhibiti ubora katika shule, utaandaliwa mpango kazi ambao utakuwa na maelekezo ya namna bora ya kusaidia watu wenye ulemavu kwanza kuibuliwa na kuingizwa katika mfumo wa elimu jumuishi.

Mdhibiti Ubora kutoka Jiji la Dodoma, Happy Gicholile alisema mafunzo hayo ni mwangaza kwao katika kuhakikisha elimu jumuishi inakuwa dira ya watoto wenye ulemavu kushirikishwa na wenzao katika kupata elimu.

Ofisa kutoka Ofisi ya Mdhibiti Ubora wa Elimu Jiji la Dodoma, Lenather Mchunguzi alisema mafunzo waliyopata watakuwa yatasaidia wao kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanasaidia watoto wenye ulemavu kupata elimu sambamba na wanafunzi wengine katika shule mbalimbali kwenye halmashauri hiyo.

Mdhibiti ubora wa elimu kutoka Bahi, Pudensia Kusenza alisema wao kama jicho la serikali katika kuhakikisha elimu inakuwa bora katika halmashauri hiyo, watasimamia kwa nguvu zote kwa kushauriana na wazazi na jamii kuwapeleka watoto katika shule ili wapate elimu jumuishi na wanafunzi wengine wasio na ulemavu.

Naye Mwanahamisi Khatibu Mdhibiti Ubora Bahi, alisema wamepata maarifa zaidi ya kujifunza namna ya kuwapa nafasi wanafunzi wenye ulemavu sambamba na wanafunzi wengine hivyo kwa kutumia nafasi zao watawasaidia watoto hao kwa kuwapa nafasi sawa na wengine.

Chanzo: habarileo.co.tz