Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waeleza kifo cha JPM kilivyowaumiza

8ef22eafa5e1d76135fe9d915f36fa50.jpeg Waeleza kifo cha JPM kilivyowaumiza

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KUFUATIA kifo cha Rais John Magufuli, wadau mbalimbali wameeleza namna rais huyo alivyokuwa na maneno ya kuwaletea maendeleo wananchi kwa kutekeleza miradi mikubwa kwa muda mfupi.

Moja ya wadau hao ni mchambuzi wa masuala ya kidiplomasia na Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia Israel Sostenes alisema Rais Magufuli alikuwa na maono makubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi.

Alisema katika katika kipindi kifupi cha uongozi wake, alifanikiwa kuifikisha nchi katika uchumi wa kati kabla ya muda uliolengwa wa mwaka 2025 uliokuwa dira ya nchi.

Kwamujibu wa mchambuzi huyo, Hayati Magufuli katika uongozi wake alitaka Tanzania iwe nchi inayojitegemea, na kuepuka utegemezi wa misaada mataifa tajiri.

“Moja ya ndoto alizofanikiwa ni pamoja na miradi mikubwa ya kimkakati mipya na iliyokuwa ikiendelea ambayo ni bwawa la kuzalishia umeme la Rufiji la Mwalimu Nyerere, Reli ya kisasa ya (SGR), ujenzi wa barabara kuunganisha maeneo mbalimbali ya nchi na barabara za juu, ununuzi wa ndege na upanuzi wa viwanja vya ndege na kuhamishia makao makuu ya nchi mkoani Dododma," alisema.

Katika uchumi, Sostenes aliwawezesha kurasimishwa kwa wajasiriamali wadogo kwa kupata vitambulisho vya ujasiriamali wakiwemo mamantilie na wamachinga.

“Ulinzi na usalama imeimarika; vitendo vya uhalifu vimepungua na udhibiti wa dawa za kulevya umeimarika, migogoro ya wakulima na wafugaji imepungua na amekuwa mstari wa mbele kukataa kasumba ya kukumbatia tamaduni za mataifa mengine zisizo na manufaa kwa jamii na pia, alidhibiti mifumo ya kiuongozi,” alisema Sostenes.

Alisema udahili wa wanafunzi katika vyuo vikuu uliongezeka, huku serikali chini ya uongozi wake ikitoa ruzuku kupitia mpango wa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, pamoja na kujenga hospitali nyingi, vituo vya afya na zahanati katika kila kijiji.

“Kuhusiana na muungano amehakikisha unaimarika na kuendelea kuondoa kasoro zilizopo pia kuleta maridhiano baina ya Wazanzibar kwa kuwakutanisha aliyekuwa kiongozi wa upinzani Maalimu Seif Sharifu Hamad (marehemu) na Dk Hussein Ali Mwinyi na hadi sasa kumekuwa na utulivu wa hali ya juu,” alisema.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) katika Mkoa wa Pwani, Abdala Ndauka alisema wamepata pigo kubwa kwa kuwa alihakikisha kunakuwa na muunganiko baina ya serikali na wafanyabiashara.

Ndauka alisema Magufuli alihimiza wafanyabiashara kuanzisha viwanda mbalimbali ili wauze hadi nje ya nchi alipopambana kuhakikisha wafanyabiashara wanaondolewa kero ili wafanye shughuli zao bila kubughudhiwa kwani mchango wao ni mkubwa kwa pato la taifa kupitia kodi na tozo mbalimbali.

Mwenyekiti wa Umoja wa Machinga Mkoa wa Pwani (UMMAPWA), Philemon Maliga, alisema wameondokewa na mpigania haki wao aliyewatetea ili wasinyanyasike katika biashara zao.

Mwenyekiti wa CCM, Kata ya Mailimoja, Mathayo Mkayala, alisema taifa limepata pigo kuondokewa na Rais Magufuli kwa kuwa alikuwa kiongozi mahiri aliyeiletea nchi maendeleo haraka.

Chanzo: www.habarileo.co.tz