Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau watoa mawazo kuhusu taka bahari

9350d1c23b81a0ac2169f0bdac668174.jpeg Wadau watoa mawazo kuhusu taka bahari

Fri, 19 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Iwapo Serikali itatafsiri sheria zinazolenga kulinda mazingira kwa Kiswahili, itasaidia kwa kiwango kikubwa wananchi wengi kuzielewa na hivyo, kurahisisha juhudi za wadau kuifanya Tanzania kuwa bora zaidi.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na maendeleo endelevu ya rasilimali za samaki na utunzaji wa makazi ya viumbe hai katika bahari, mito na maziwa la Aqua Farms Organisation (AFO), Jerry Man’gena, amesema hayo leo Dar es Salaam katika kikao cha wadau mbalimbali wanaohusika na kuelimisha jamii na kutokomeza taka bahari.

Mbali na kutafsiri sheria hizo, Man’gena alisema upo umuhimu pia wa kuzioanisha sheria kadhaa zinazogusa masuala ya mazingira ili kuondoa baadhi ya migongano iliyopo miongoni mwa sheria hizo ili kuleta ufanisi zaidi.

“Zipo sheria za uvuvi, mazingira, maji… Hizi zote zinatakiwa kuoanishwa ili kuwa na lengo moja linapokuja suala la kulinda mazingira ya bahari,” alisema na kuongeza kuwa, panatakiwa kuwa na mabadiliko ya mtazamo na kuwafanya wananchi kuwa na utayari, ushiriki na umiliki wa programu za usafi si wa bahari tu, bali na nchi kavu.

Alisema asilimia 80 ya uchafu wa bahari huanzia maeneo ya mbali na bahari.

Hayo yanabainika katika utafiti uliofanywa na AFO kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Elizade kwa ufadhili wa Association of Commonwealth University uliolenga kuhabarisha wadau juu ya mitazamo ya watu kuhusu taka bahari katika kanda za Pwani za Dar es Salaam, Bagamoyo na Zanzibar.

Zaidi ya watu 200 walihojiwa katika utafiti huo.

Kikao hicho kililenga kujadiliana na kukusanya maoni ya wapi pa kuongeza nguvu ili kutokomeza mitazamo hasi inayohatarisha viumbe vya baharini, kizazi cha sasa na siku zijazo.

Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Kinondoni, Grace Kakana, alisema utafiti huo umekuja wakati sahihi kwani unaongeza nguvu katika juhudi zinazofanywa na serikali na Kanda ya Afrika ya Mashariki kupambana na taka bahari na maeneo ya mito na maziwa.

“Taka bahari ni tishio,” alisema Kakana na kuongeza kuwa, utafiti kama huo ni muhimu katika kupambana nazo.

Nyakorema Rioba ambaye ni, mwanzilishi wa Shirika la Eeco-Initiative, alisema hata kama Tanzania si moja ya nchi 20 duniani zinazoongoza kwa tatizo la taka bahari, bado kuna changamoto kubwa.

Moja ya changamoto hizo, alisema, ni kukosekana kwa data zinazoonesha kwa mfano, kiasi cha taka kinachozalishwa na mtu mmoja.

Alisema mapambano dhidi ya taka bahari yanahitaji mshikamano wa wadau mbalimbali kama serikali, wananchi, viwanda na mashirika yanayohusika na elimu.

“Ili kufanikiwa, kila mtu atimize wajibu wake katika nafasi yake,” alisema.

Katibu wa Umoja wa Wavuvi eneo la Msasani, Dar es Salaam, Hujeje Mamboleo, alisema serikali inatakiwa kuliangalia suala la taka bahari kwa jicho la pili kwani wao kama wavuvi, hushuhudia madhara makubwa kwa samaki na uharibifu wa injini za boti za uvuvi kutokana na plastiki baharini.

“Samaki kama chewa na kasa, hula sana plastiki. Athari ni kubwa, wenye mamlaka walishughulikie sana suala hili,” alisema Hujeje.

Alisisitiza umuhimu wa kutoa ushirikiano stahiki kwa wadau wanaofanya tafiti kama uliofanywa na shirika hilo la AFO.

Awali, akiwasilisha mada kwa wadau hao, Mkurugenzi wa Tafiti na Miradi wa AFO, Fadhili Malesa, alisema wengi waliohojiwa walikubali kuwa tatizo la taka bahari lipo na kuwa ni tishio kwa usalama wa bahari.

Hata hivyo, baadhi ya waliohojiwa walisema plastiki huchukua miaka mitano kuoza wakati ukweli ni kwamba, huchukua miaka 4,500 mpaka kuanza kuvunjikavunjika.

Alisema utatuzi wa tatizo la taka bahari unatakiwa kushirikisha hata watu wanaoishi mbali na fukwe kwani hao pia huzalisha taka zinazosafirishwa hadi baharini.

wakitoa mawazo yao, baadhi ya wadau katika kikao hicho walisema elimu zaidi itatakiwa kuanzia ngazi ya familia na shuleni ili watoto wajifunze wangali wadogo kuhusu umuhimu wa mazingira safi.

“Elimu hii ya mazingira iingizwe katika mitaala ya elimu mapema,” alisema Bw. Zagalo Emmanuel kutoka Arena Recycling Industries.

Farida Muslim wa Mazingira Plus, alisema pawe na mwendelezo wa mipango ya mazingira inayoanzishwa, sheria za mazingira zifuatwe na kutekelezwa na pia, mamlaka zitumie taarifa za utafiti unazofanywa na wadau kuboresha mazingira.

Chanzo: www.habarileo.co.tz