Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadau wakosoa mbinu za kudhibiti ukahaba Dar

#VIDEO: DC Kinondoni Alivyowadaka Machangudoa Wadau wakosoa mbinu za kudhibiti ukahaba Dar

Mon, 6 Nov 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mbinu zinazotumiwa na Serikali jijini Dar es Salaam kukomesha biashara ya ukahaba zimekosolewa, huku wachambuzi wakiitaka ianze kuangalia mzizi wa tatizo, badala ya kuwakabili wahusika wa vitendo hivyo.

Kulingana na wachambuzi hao ambao pia watetezi wa haki za binadamu na wanasheria, ni muhimu kuzikabili sababu zilizowafanya wajihusishe na biashara hiyo na si kuwakabili wenyewe, wakisisitiza utafiti ni jambo la msingi kabla ya kuanza operesheni hizo.

Hata hivyo, ukosoaji huo wa wadau umejibiwa na Serikali ikisema, haikukurupuka kufikia uamuzi wa kufanya operesheni ya kutokomeza madanguro na biashara hizo, bali ilifanya stadi tangu Machi, mwaka huu.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule , alisema pamoja na sababu zilizobainika, si kigezo cha watu hao kutweza utu wao.

Hayo yanajiri ikiwa ni wiki mbili tangu Serikali wilayani Kinondoni ianze operesheni ya kutokomeza madanguro na biashara ya ukahaba.

Hatua hiyo ya Wilaya ya Kinondoni iliungwa mkono na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Dar es Salaam, Albert Chalamila aliyefanya ziara za kushtukiza katika madanguro mbalimbali na kudhibiti vitendo hivyo.

Hata hivyo, udhibiti wa biashara hizo jijini hapa unaonekana kuwa mfupa mgumu uliowashinda viongozi wengi, kwa sababu Chalamila si kiongozi wa kwanza kutangaza na kufanya operesheni hizo, iliwahi kufanywa hivyo na Paul Makonda aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, lakini juhudi zake hazikuzaa matunda.

‘Tutafiti chanzo’

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, alisema ni muhimu kufanywa utafiti wa kujua chanzo cha wanawake hao kujihusisha na shughuli hizo badala ya kutumia nguvu.

Akizungumza na Mwananchi jana, Ole Ngurumwa alisema chanzo hicho kisiangaliwe kwa wanaouza pekee, ni vema iangaliwe kwa nini wanaume pia wanakwenda kununua kwa wauzaji hao.

“Tunapaswa kuangalia uwepo wao umesababishwa na nini, kabla ya kuwakamata na kuwafukuza. Ukiangalia asilimia kubwa ni wale wenye maisha magumu, walitelekezwa, wana watoto wanahitaji huduma,” alisema.

Kulingana na Ole Ngurumwa, kuvunja madanguro ni kutoa mwanya kwa biashara hiyo ifanyike kwa mtindo wa kujipanga barabarani.

Alisema hatua hiyo ndiyo mbaya zaidi kwa kuwa itaathiri wengi hata wale wasiokuwa watumiaji.

“Wakati mwingine ni bora kuwa na maeneo kama hayo kuliko kukaa barabarani, kwa sababu si kila mtu anahitaji. Tungedhibiti zaidi hii ya kukaa barabarani, lakini kunapokuwa na sehemu maalumu inaweza kufanya hivyo vitu visifanyike hadharani na kuharibu utamaduni zaidi,” alisema.

Hata hivyo, alisema zipo athari nyingine kwa binadamu iwapo madanguro hayo yatavunjwa, akifafanua zilikuwa nyumba za watu na ndiyo msingi wa kipato chao.

Katika hatua nyingine, Ole Ngurumwa alisema pengine uwepo wa huduma hizo ni ahueni ya kutokea kwa majanga mengine, kama ubakaji na watoto kuingiliwa.

“Kwa sababu kuna nafasi ya watu kwenda kutuliza mihemko yao ya kibaiolojia, kuna vitu vingine vipo kwenye jamii kwa ajili ya ku-balance maisha,” alisema.

Ingawa hakuthibitisha, lakini alisema uwepo wa biashara hizo katika maeneo ya miji pengine ndiyo sababu hata vitendo vya ubakaji vimepungua na kwa sasa vimebaki zaidi vijijini ambako hakuna huduma hizo.

Wengi wanafanya kwa siri

Kwa msingi wa ufafanuzi wa sheria ya makosa ya jinai ulioelezwa na Ole Ngurumwa, watu wengi wanafanya shughuli za ukahaba ingawa hawajaweka hadharani.

Alieleza sheria hiyo inalitafsiri kosa la ukahaba kuwa tendo lolote la kujipatia fedha kwa njia yoyote ya ngono.

“Kwa maneno mengine kama uliwahi kufanya ngono ili upate fedha huo ni ukahaba,” alisema.

Lakini, alieleza ugumu wa ushahidi wa kosa hilo kwa kuwa si rahisi kumkuta mtu anapokea fedha na ukathibitisha imetokana na tendo la ngono.

‘Ilihitajika busara’

Mkurugenzi wa Uchechemuzi na Maboresho wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe alisema kulihitajika busara na hekima katika hatua dhidi ya wanaofanya biashara ya ukahaba, tofauti na inavyofanywa sasa.

Alikiri biashara hiyo ni kinyume cha sheria, lakini mbinu inayotumika kuidhibiti inavunja maadili na kuwadhalilisha watuhumiwa.

“Wanapokwenda wanawahoji wanachukua video zinarushwa na vyombo vya habari, ni kosa la kimaadili kwa sababu wapo watu ambao hawajui kama kuna vitendo hivyo unapowaonyesha sio sawa,” alisema.

Hivyo, kulingana na mazingira ya kisheria, Massawe alisema ni vigumu kukabiliana na vitendo hivyo, akidokeza ndiyo sababu watuhumiwa wengi huishia kushtakiwa kwa kosa la uzururaji.

Kingine kinachoweka ugumu, alisema ni namna ambavyo shughuli hiyo hufanyika, akifafanua mbali na wanaofanya kwenye madanguro, wengine hufanya kupitia mtandao na wapo wanaofanya wakiwa nyumbani.

Maoni ya wateja

Katika mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari, baadhi ya wateja katika moja ya danguro jijini Dar es Salaam, alilalamikia uamuzi huo wa Serikali wakisema wanaonewa.

“Sisi tufanye madhara mtaani? Sisi tunaishi nao, tukiwa na Sh3,000 tunaenda nao sawa, hatutaki kesi,” alisema mmoja wa wateja hao bila kutaja jina.

Mwingine alisema, “Mimi naona tunaonewa kutokana na kwamba hawa wanatusaidia, hatutaki kuharibu watoto wadogo na wake za watu, ndiyo maana hawa wanatusaidia matatizo yetu tunamaliza,” alisema.

Utetezi wao dhidi ya machangudoa, unatokana na kile kilichoelezwa na baadhi yao kuwa, kwa kiasi kikubwa wanaofanya shughuli hizo ni salama dhidi ya magonjwa.

“Siku zote wapimaji (Virusi vya Ukimwi) wanakuja huku na hawa (machangudoa) huwezi kufanya nao mapenzi bila kuvaa kondomu, kwa hiyo usalama ni uhakika, bila kondomu hakubali.

“Wakiondoka hawa sisi tutafanyaje, mtoto wa kiume mwenyewe unaelewa zikipita siku kadhaa unataka upunguze,” alisema.

Viongozi wa kimila

Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu Tanzania, Tonisiza Antonia alisema shughuli hizo si njema kwa misingi ya maadili, lakini Serikali inapaswa kutafuta mbinu stahiki za kudhibiti.

Alipendekeza miongoni mwa mbinu hizo ni kuwaorodhesha majina na kuwawezesha kulingana na mahitaji ya kila mmoja, ili wawe na njia mbadala ya kujipatia fedha.

“Kuvunja nyumba wanazofanyia shughuli hizo nisiliongelee sana, lakini Serikali inapaswa kuwatafutia shughuli mbadala, isiishie kuwazuia iwatafutie shughuli itakayowawezesha kupata fedha na kama wanafanya kwa hulka itajulikana,” alisema.

Serikali: Hatukukurupuka

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mtambule alisema hawakukurupuka kuchukua uamuzi huo, kwani ni jambo lililoanza kwa stadi iliyofanyika tangu Machi, mwaka huu.

“Tulifanya utafiti wa kutosha juu ya mmomonyoko wa maadili ndani ya wilaya yetu na vyanzo vyake na tulijiridhisha juu ya visababishi vyake,” alisema.

Pamoja na visababishi hivyo, Mtambule alisema si kigezo cha watu kutweza utu wao.

Stadi iliyofanyika kwa mujibu wa Mtambule ilihusisha mazungumzo na wamiliki wa madanguro, viongozi wa dini, wadau wa haki jinai, maofisa ustawi wa jamii, makahaba na wananchi.

“Mei mwaka huu nilifanya kikao na wamiliki wa madanguro na tuliyajua yote, mahali yalipo na wamiliki wake kwa hiyo hadi tunafanya operesheni hii hatukukurupuka,” alisema.

Hata hivyo, alieleza kinachofanywa sasa ni kuangalia namna ya kuwaunganisha na waliokuwa wanafanya biashara hizo na fursa mbalimbali zilizopo wilayani humo.

Akizungumzia wamiliki wa majengo hayo, mkuu huyo wa wilaya alisema wamewataka wayatumie kulingana na matakwa ya hati za umiliki na ikibainika wanakiuka sheria, watakwenda mahakamani kwa ajili ya kuyataifisha.

Chanzo: mwanachidigital