Shirika la HakiElimu limelaani kitendo kilichofanywa na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kakanja mkoani Kagera ambaye katika kipande kifupi cha video anaonekana akiwacharaza bakora wanafunzi wawili kwenye nyao za miguu huku wakiwa wamevua viatu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 26, 2022 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, John Kalage amesema kitendo hicho kinakiuka sio tu haki za watoto bali pia ni kinyume na maadili ya kazi ya ualimu na malezi bora ya wanafunzi.
Hata hivyo Kalage ameipongeza serikali kwa kuchukua hatua za awali kwa haraka dhidi ya mwalimu aliyetenda tukio hilo ikiwemo kumvua nafasi yake ya Ualimu Mkuu, kumsimamisha kazi na kuunda tume ya kuchunguza tukio hilo ili hatua za kisheria ziweze kufuatwa.
"Tunaipongeza serikali kwa hatua za haraka zilizochukuliwa dhidi ya aliyefanya tukio hilo la kikatili kwa wanafunzi hao wawili, "anasema.
Alisema tukio hilo linakumbusha matukio kadhaa ya ukatili wa vipigo dhidi ya wanafunzi ikiwemo lile lililotokea mwaka 2016 katika Shule ya Sekondari ya Kutwa huko Mbeya ambapo walimu watatu kwa pamoja waliripotiwa kumpa adhabu ya viboko na ngumi mwanafunzi na kusababisha kulazwa hospitali.
"Mwaka 2018 mwanafunzi Sperius Eradius wa Shule ya Msingi Kibeta mkoani Kagera alifariki kutokana na adhabu ya viboko kutoka kwa mwalimu wake," amesema.
Anasema katika utafiti uliofanywa na shirika hilo mwaka 2020 takribani asilimia 87.9 ya watoto shuleni waliripoti kufanyiwa ukatili wa kimwili huku asilimia 90 kati ya hao ulitokana na adhabu za viboko zinazotolewa shuleni.
"Katial utafiti huu asilimia 54.9 ya watoto walisema walimu wao na walezi wanatumia kupiga ngumi na makofi kama sehemu ya adahabu ," anasema.
Akizungumza na wanahabari jana Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila ameeleza sababu ya mwalimu huyo kuwapa adhabu wanafunzi kuwa walikataa kufanya zoezi/maswali waliyopewa waifanyie nyumbani wakati wa likizo hivyo akawapa adhabu kwa kuwachapa viboko kwenye nyayo za miguu huku akiwa amewakanyanga miguu yao.
Chalamila alisema kuwa, richa ya kumchukulia hatua mwalimu mkuu huyo pia walimu wanne waliokuwa ofisini hapo wamechukuliwa hatua za kusimamishwa kazi kwa kutomshauri mwalimu mkuu juu ya adhabu aliyokuwa akitoa kwa wanafunzi wawili wa darasa la nne ambao ni Salmon Kakwezi miaka tisa na Anord Kweyamba (10) ambao richa ya kumuomba msamaha lakini hakuweza kuwasamehe na walimu hao walikuwa wakicheka na kufurahi.