Wadaiwa sugu wa nyumba za makazi za Wakala wa Majengo Tanzania (TBA,) wameanza kuondolewa katika nyumba hizo na dalali wa Mahakama baada ya kushindwa kulipa kodi ya pango hali iliyokwamisha jitihada za Wakala hiyo katika utekelezaji wa na uboreshaji wa miradi ya namna hiyo kwa manufaa ya Umma.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi la kuwaondoa wakazi katika nyumba za TBA, Mbezi Beach Jijini Dar es Salaam; Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Dar es Salaam Arch. Benard Mayemba amesema, zoezi hilo limekuja baada ya rai iliyotolewa na Mtendaji wa Wakala hiyo juu ya namna bora ya kuwaondosha wapangaji wenye madeni sugu katika nyumba hizo za TBA.
" Wapangaji hawa ambao ni watumishi wa Umma wamepewa fursa ya kukaa lakini wamekuwa wakaidi katika kulipa kodi kama ilivyoelekezwa....Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtendaji Mkuu kwa vyombo vya habari hivi karibuni alieleza kuwa zoezi hili litaanza tarehe moja mwezi kwa 12 lakini kwa Mkoa wa Dar es Salaam zoezi hili limeanza leo kwa kuwa zoezi la kutoa notisi lilifanywa siku kumi zilizopita na dalali wa Mahakama WINS Auction Mart, hivyo baada ya siku za notisi kuisha zoezi la kuwaondosha wadaiwa sugu limeanza." Amesema.
Amesema Mkoa wa Dar es Salaam una nyumba zaidi ya 1200 na wafanyakazi wa Umma wamepata nafasi ya kukaa katika nyumba hizo lakini wengi wao wamekiuka taratibu kwa kulimbikiza madeni hadi kufikia shilingi Bilioni 1.1.
"Hatua tuliyochukua ya kumtumia dalali wa Mahakama katika zoezi hili litakalochukua wiki tatu.....zoezi hili halitaangalia wadhifa, rika wala muonekano yeyote anayedaiwa kodi ataondolewa ili watumishi wengine wapate fursa ya kupata makazi." Amesema.
Aidha amesema, utekelezaji wa zoezi unaisaidia Wakala hiyo kupata fedha ambazo zitaelekezwa katika kufanya marekebisho ya majengo na miundombinu ya majengo hayo pamoja na kutekeleza miradi mingine itakayopunguza changamoto za makazi.
Kuhusiana na changamoto ya makazi Mkoani Dar es Salaam Arch. Mayemba amesema kuwa, kupitia zoezi hilo mapato yatakayokusanywa pia yataelekezwa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika jiji hilo kupitia makusanyo ya ndani.
Jumla ya wadaiwa sugu 118 katika maeneo ya Mbezi Beach, Masaki, Oysters bay, Ilala, Temeke na Chang'ombe jijini Dar es Salaam wataondolewa katika nyumba hizo na kuchukuliwa hatua za kisheria huku zoezi hilo likitarajiwa kuanza Desemba Mosi mwaka huu katika Mikoa yote ambayo imefanya deni kufikia shilingi Bilioni 7.8 huku taasisi za Serikali zikidaiwa takribani Bilioni 3.5.