Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadaiwa kutoa barua za utambulisho kwa wasio wajua

Pcb Mbeya Wadaiwa kutoa barua za utambulisho kwa wasio wajua

Fri, 18 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mara imebaini uwepo wa baadhi ya watendaji wa vijiji wilayani Butiama kutoa barua za utambulisho wa vyeti vya kuzaliwa kwa watu wasiowafahamu.

Taasisi hiyo pia imebaini uwepo wa baadhi ya wasaidizi wa ofisi ya Katibu Tawala Wilaya ya Butiama kupokea fedha taslimu kutoka kwa waombaji wa vyeti vya vizazi na vifo kinyume cha sheria na taratibu.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi kwa mwezi Aprili hadi Juni mwaka huu leo Alhamisi Agosti 17, 2023 Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Anthony Gang'olo amesema vitendo hivyo vimebainika baada ya ofisi yake kufanya uchambuzi wa mfumo wa usajili wa vizazi na vifo wilayani humo.

“Watendaji wanasaini barua za watu wasiowajua hii ni hatari sana kwa usalama wa nchi kwani hawa watu wasiojulikana wanaweza kupata uraia baada ya kupewa vyeti vya kuzaliwa na vitambulisho vya taifa,”amesema Gang'olo

Kuhusu wasaidizi wa ofisi ya Katibu tawala, Gang'olo amesema kwa mujibu wa taratibu wasaidizi hao wanatakiwa kutoa namba ya malipo badala ya kupokea pesa taslimu hali ambayo inaashiria uwepo wa malipo zaidi ya kiwango kinachotakiwa.

“Pia tumebaini udanganyifu kwenye utaoji wa vyeti vya vizazi na vifo mfano kuna mtu alifariki lakini ofisi ya vizazi na vifo ikatoa vyeti viwili tofauti kwa kifo kimoja kinyume cha sheria na taratibu,”amesema

Kufuatia hali hiyo Takukuru imeelekeza barua za maombi ya vyeti vya kuzaliwa kuandikwa na watendaji wa Kata kwa usaidizi wa karibu na wenyeviti wa vitongoji huku Katibu Tawala akitakiwa kusimamia utoaji wa vyeti vya vizazi na vifo yeye mwenyewe badala ya wasaidizi wake.

Katika hatua nyingine taasisi hiyo imefanya ukaguzi wa miradi 43 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh15.4 bilioni katika sekta za barabara, elimu, biashara, maji na Utawala.

Gang'olo amesema miradi mitatu kati ya hiyo yenye thamani ya zaidi ya Sh700 milioni ilibainika kuwa na kasoro na hivyo kuamuru kasoro hizo zirekebishwe kabla ya miradi kuendelea.

Wakati huo huo taasisi hiyo katika kipindi hicho imepokea jumla ya malalamiko 114 ambapo 71 yalihusu vitendo vya rushwa huku kesi tatu zilifunguliwa mahakamani na kufikisha kesi 29 zinazoendelea Mahakamani

Chanzo: www.tanzaniaweb.live