Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wadai tuta la SGR limeleta mafuriko Morogoro

Tuta Tuta Tutaaaa.png Wadai tuta la SGR limeleta mafuriko Morogoro

Thu, 1 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mafuriko yaliyoikumba Kata ya Kihonda na Lukobe katika Manispaa ya Morogoro, yamewagusa wananchi moja kwa moja na baadhi yao wameyahusisha na kujengwa tuta la reli ya kisasa pamoja na makaravati yake madogo.

Wakazi hao wamesema miundombinu hiyo imezuia mtiririko wa maji yaliyokuwa yanapita katika njia zake za asili, badala yake yameelekea kwenye makazi ya watu.

Hata hivyo, hakuna mamlaka iliyokiri kuwepo uhusiano huo, huku msemaji wa Shirika la Reli akisema alikuwa kwenye kikao.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TRC, Jamila Mbaruku akizungumzia madai hayo alijibu yupo kikaoni na kuahidi kumrudia mwandishi pale atakapomaliza kikao hicho na alipotafutwa kwa mara nyingine simu yake iliita bila majibu.

Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Rebeca Nsemwa alipotafutwa azungumzie hilo, alisema “mafuriko yametokana na mvua za El-Nino zilizotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA).”

Nsemwa alipingana na kauli ya wakazi wa kata hiyo kuwa yamesababishwa na tuta la reli.

Alisema TMA ilishatangaza uwezekano wa kuwepo mvua kubwa katika maeneo mengi nchini na Morogoro ikiwemo na athari zake ni pamoja na kutokea kwa mafuriko.

“El-Nino maana yake ni uwepo wa mvua kubwa zinazonyesha mfululizo na ndicho kinachotokea hapa Morogoro, tayari tulishawashauri wananchi watoke kwenye maeneo ya mikondo ya maji na mabondeni, lakini walitupuuza wakidai utabiri huo si wa kweli, halafu wanakuja na kauli tofauti. Haya mafuriko wala hayajasababishwa na hilo tuta la mwendo kasi,” alisema.

“Watu wa Kihonda wanasema mafuriko yamesababishwa na tuta la reli, mbona hata kabla ya tuta kujengwa yalishawahi kutokea tena mafuriko kama haya, nayo yalisababishwa na tuta wakati halikuwepo? Na kuna maeneo mengine hapahapa Morogoro tuta hilo wala halijajengwa, mbona yamekumbwa na adha hii?” alihoji.

Alitolea mfano Kata ya Mafisa na maeneo ya katikati ya mji ambayo yamekumbwa pia na mafuriko bila kuwepo kwa tuta.

Waathirika wafunguka

Akizungumzia mafuriko hayo yaliyotokea Kihonda na Lukobe, mkazi wa Mtaa wa Kihonda B, Aziz Msuya alisema chanzo cha mafuriko hayo ni kujengwa kwa tuta la reli pamoja na makaravati madogo aliyodai yanashindwa kupitisha maji mengi na kusababisha yatawanyike kwenye makazi ya watu.

Alidai baadhi ya mamlaka na viongozi wanakwepa kuzungumza ukweli kuhusu chanzo, badala yake wanazungumzia mikakati ya kurudisha miundombinu iliyoharibika, suala alilosema si mwarobaini wa tatizo.

Msuya ambaye amelazimika kuihama nyumba yake kutokana na mafuriko hayo, alisema hajawahi kuyashuhudia muda wote wa miaka 17 alioishi katika eneo hilo.

Alisema inawezekana waliopewa dhamana ya kufanya tathmini ya matokeo ya athari za kimazingira hawakufanya sawasawa.

“Pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoelezwa na baadhi ya mamlaka na viongozi wa siasa, ujenzi wa tuta hilo umechangia kutokea kwa mafuriko ya mara kwa mara katika manispaa hiyo.

Msuya alisema miaka ya nyuma, mvua kubwa zilikuwa zikinyesha lakini hakukuwa na mafuriko ya aina hiyo, bali yameanza kutokea baada ya kujengwa tuta hilo la reli.

“Ilikuwa mvua zikinyesha hata ziwe kubwa kiasi gani, lakini sasa hivi mvua ikinyesha tu maji yanashindwa kupita kwenye njia zake za asili yanatawanyikia kwenye makazi ya watu,” alidai Msuya.

“Wataalamu walipaswa kujenga reli hiyo kwa kutumia nguzo ili kuruhusu maji yapite kwenye njia zake badala ya kujenga tuta hili ambalo sasa hivi linasababisha madhara na uharibifu wa mali za watu kutokana na mafuriko,” alidai mkazi huyo.

Mkazi wa Mtaa wa Azimio, Plaxeda Malya alisema ameishi eneo hilo kwa zaidi ya miaka 10 na hajawahi kushuhudia mafuriko kama yaliyotokea mwaka huu.

“Mimi naamini mafuriko haya yametokana na miundombinu duni iliyowekwa na wataalamu waliojenga tuta la reli ya mwendo kasi, makaravati waliyoweka yanashindwa kupitisha maji mengi,” alidai Malya.

Alisema watu wamepoteza mali nyingi, huu akijitolea mfano kuwa vyombo anavyotumia kwenye shughuli zake za biashara ya chakula vyenye thamani ya Sh9 milioni vyote vimesombwa na mafuriko.

“Siku ilipotokea mafuriko haya nilikuwa nina kazi kubwa tatu ya kutoa huduma ya chakula, mvua ilipoanza nilikuwa nimeshapakua vyakula na kuweka kwenye vyombo tayari kwa kupeleka kwa wateja, nilishindwa na chakula chenyewe pamoja na vyombo vyake vikasombwa vyote,” alisema Malya.

Kwa upande wake Moses Mbinde alisema licha ya kunufaika na uwepo wa reli ya kisasa, walioijenga walipaswa kuzingatia ubora wa reli na maisha ya watu wanaoishi jirani na reli hiyo.

“Maafa ni makubwa, Serikali isinyamazie wala kupuuzia jambo hili, kwa sababu ipo siku itapeperusha bendera nusu mlingoti kutokana na maafa, nashauri kama itashindwa kurekebisha hili tuta la reli, basi waje na mkakati wa kuwalipa fidia wananchi waondoke kabisa maeneo haya,” alisema Mbinde.

Aliishauri halmashauri kutafuta mahali pa kuwahifadhi waathirika wa mafuriko hayo badala ya kuwaacha waendelee kuishi katika “maeneo hatarishi”.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Azimio, Michael Bendera tangu mwaka jana hali ya mafuriko ilianza kujitokeza na alishatoa taarifa kwenye kata na hata kwa wataalamu wa mazingira, lakini hakuna kilichofanyika mpaka sasa.

Bendera alisema mpaka sasa nyumba 25 zimebomoka na kaya zaidi ya 320 zimekosa mahali pa kuishi, huku naye akiyahusisha na tuta la reli, licha ya kuwepo kwa sababu nyingine kama mabadiliko ya tabianchi na mvua za El- Nino.

Akizungumzia suluhisho, Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga alisema mwarobaini ni wataalamu wa ujenzi wa reli ya mwendokasi kurejea katika eneo la mradi na kufanya tathmini upya.

Kihanga alisema tayari manispaa imefanya tathmini ya awali na kuona njia ya haraka ni kujenga mitaro mikubwa minne, itakayopitisha maji bila vikwazo kuelekea Mto Ngerengere.

“Lakini pia kuweka makaravati katika barabara zinazopita katika mitaa, ila tunahitaji fedha ambazo tutawahamisha watu ambao watapisha ujenzi wa mifereji na kulipwa fidia na tutawapa viwanja bure ambavyo Manispaa wanauza hasa kule Kiegea,” alisema Kihanga.

Alisema halmashauri iliwaamuru maofisa watendaji kata kutumia ofisi za serikali ya mtaa, kata kuwahifadhi watu ambao nyumba zao zimebomoka kabisa.

Hata hivyo, alisema kuna umuhimu kwa Serikali na wataalamu kufanya tathmini sahihi ili kuboresha miundombinu na kuchukua hatua za kuzuia mafuriko kwa siku zijazo katika maeneo yote yaliyoathirika.

“Pia, ni muhimu kwa jamii kuchukua tahadhari na kushirikiana na mamlaka husika katika kupunguza athari za mafuriko,” alisema Meya huyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live