Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachina 97 waliokamatwa wakifanya kazi bila vibali watozwa faini ya Sh654 milioni

Wachina 97 waliokamatwa wakifanya kazi bila vibali watozwa faini ya Sh654 milioni

Wed, 30 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Geita.  Wachina  97 waliokamatwa Oktoba 22, 2019 mkoani Geita katika mgodi wa dhahabu wa Nyamahuna kwa madai ya kufanya kazi nchini bila kuwa na kibali wametozwa faini ya Sh654 milioni.

Akizungumza leo Jumatano Oktoba 30, 2019 mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel amesema raia hao wa kigeni wamekutwa wakifanya kazi bila kibali, kukwepa kodi na kukiuka taratibu za uchimbaji madini.

Amesema  Mkoa huo unahitaji wawekezaji lakini lazima wajiridhishe kuhakikisha taratibu za nchi zinafuatwa, kubainisha kuwa faini zilizolipwa ni tozo za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), idara ya uhamiaji na idara ya kazi.

Amewataka watendaji Wizara ya Madini na TRA kukaa na wananchi wenye leseni za uchimbaji walioingia ubia na wawekezaji ili kuona namna ya kuboresha mikataba hiyo kwa faida ya wenye leseni, wawekezaji na Serikali

Francis Kiganga, mwanasheria wa mgodi wa RZ Union ambao ni sehemu ya  mgodi wa Nyamahuna  amesema Wachina hao hufika katika mgodi huo kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji.

“Mkuu wa Mkoa mchimbaji mdogo akiingia kazini akilipwa kesho haji anatumia fedha hadi ziishe ndio hurudi tena. Kiutendaji si nzuri ndio maana umeona Wachina nao wanaingia shimoni wanafanya kazi na wako vizuri, “amesema Kiganga. Ofisa kazi wa Mkoa wa Geita, Mohamed  Majaliwa amesema baadhi ya mambo waliyoyabaini kwenye mgodi huo ni mwajiri kutokuwa na mikataba ya ajira, kumbukumbu ya kuingia na kutoka kazini, kumbukumbu ya mgawanyo wa kazi .

AmEsema pia mwajiri amekutwa hana hati ya malipo ya mshahara pamoja na kutojisajili kwenye mifuko ya jamii.

Kaimu Meneja wa TRA Geita,  John Njau amesema kukosekana kwa rekodi za ajira, mishahara na kumbukumbu zinazoonyesha utendaji kazi wa watumishi zimechangia upotevu wa kodi za waajiri na waajiriwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz