Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wachimbaji wadogo Kigoma wakumbushwa kufuata sheria

C6c857208588387513d70dde5884b2e1 Wachimbaji wadogo Kigoma wakumbushwa kufuata sheria

Sat, 13 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

WACHIMBAJI wadogo na wafanyabiashara wa madini mkoani Kigoma wametakiwa kufuata sheria na taratibu za uchimbaji na uuzaji madini ili kuondoa migogoro baina yao na serikali hasa katika ulipaji kodi.

Mkuu wa wilaya Kasulu, Simon Hanange akifungua mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini mkoani humo alisema kuwa wachimbaji wengi na wafanyabiashara ya madini wanapenda kufanya shughuli zao kwa njia za panya ili waweze kukwepa kulipa Kodi.

Hanange alisema kuwa wafanyabiashara hao kufanya shughuli zao kwa njia na taratibu halali kunawawezesha kufanya shughuli zao kwa kujiamini lakini pia kupata usaidizi kutoka serikalini na taasisi za fedha kupata mikopo na ruzuku kwa ajili ya kuendelea shughuli za uchimbaji na biashara ya madimi.

Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa serikali inawaunga mkono na ndiyo maana baada ya kikao cha Rais Magufuli na wadau wa madini tozo 23 ziliondolewa ili kuwapa nafuu wachimbaji na wafanyabiashara ya madini kufanya shughuli zao kwa tija.

Awali akitoa maelezo kuhusu mafunzo hayo ofisa biashara katika sekretarieti ya mkoa Kigoma, Deogratius Sangu alisema kuwa mafunzo hayo yamewahusisha wachimbaji wa madini mbalimbali ikiwemo dhahabu na chokaa na wafanyabiashara wa madini kutoka wilaya zote za mkoa Kigoma.

Sangu alisema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwapa uelewa wachimbaji na wafanyabiashara hao kuhusu sheria na taratibu zinazoongoza shughuli zao na namna ya kufanya shughuli hizo kuwa na tija ikiwemo namna ya kutambua Masoko yaliyopo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Asha Poroto muuzaji wa chokaa mjini Kigoma alisema kuwa katika siku ya kwanza ya mafunzo hayo wamejua vitu vingi kuhusiana na shughuli ya madini ambapo hapo awali hawakuwa wanavijua.

Poroto alisema kuwa kujua sheria na taratibu za madini kutawaondolea migogoro ya mara kwa Mara na wasimamizi wa shughuli za madini wakiwemo wakala wa misitu, masuala ya mazingira, afya, usalama kazini na ulipaji tozo na Kodi mbalimbali ambazo wamekuwa wakilalamikia

Hata hivyo mmoja wa wachimbaji wadogo wa dhahabu kutoka wilaya ya Kakonko, Joyce Masika alilalamika vifaa duni wanavyofanyia kazi huku kukiwa na shida kubwa ya kupata uwezeshaji na mikopo kutoka taasisi za fedha na halmashauri hivyo kufanya shughuli zao katika mazingira magumu na ya hatari.

Chanzo: habarileo.co.tz