Wachimbaji 22 waliofia mgodini Bariadi watambulika Mwanza. Wachimbaji wadogo 22 waliofariki dunia katika ajali ya kuangukiwa na gema ndani ya mgodi wa Ikinabushu wilayani Bariadi, mkoani Simiyu wametambulika.
Ajali hiyo ilitokea saa 11 alfajiri ya kuamkia Januari 13, 2024 baada ya wachimbaji hao kudaiwa kuingia ndani ya mgodi ambao shughuli zake zimesitishwa na wakaguzi kutoka Ofisi ya Madini Mkoa wa Simiyu kutokana na ukiukwaji wa taratibu za kisheria ikiwemo eneo la uchimbaji kutokuwa salama.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Jumatatu Januari 15, 2024, Kaimu Kamanda wa Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, Faustine Mtitu ametaja majina ya waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Duasi Ndaki (28), Magembe Sita (30), Mussa Shinyanga (32), Sono Sayi (33) na Mshona Mbooma (41).
Wengine waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea ni Tui Nhandi (30-35), Kichiba Masunga (24), Ngaba Inuka (31), Makolo Nyangihimbu (30-35) na Dotto Weda (25-30).
Kaimu Kamanda Mtitu amewataja marehemu wengine kuwa ni Nyahoka Chacha (33), Mayala Maendeleo (35), Komiga Maduhu (29), Sayi Zanzibar (20), Doya Kiuma (25-30), Kija Lubana (30-35), Kimeli Chabozi (29) na Joel Matiku (26).
Katika orodha hiyo pia wamo Maduhu Sungi (22), Toroto Gregorl (32), Kilindo Nyamhanga (44) na Jumanne Sondobhi anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kato ya 30 hadi 35.