Moshi. Kama hauko katika koo zilizotawala zamani za kina Mangi unaweza kupatwa na mshangao. Katika koo hizi hadi sasa ufukuaji wa mabaki ya wapendwa wao waliozikwa zaidi ya miaka 10 iliyopita bado unafanyika.
Huu ni utamaduni ambao hata kwa wenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro, mahali kuliko na koo hizo zilizotawala miaka mingi iliyopita, bado wanaushangaa.
Koo hizo za Kabila la Wachaga zinafukua mabaki hayo ya miili, lakini si zote, ingawa kwa wanaofukua wanafanya hivyo kwa malengo mawili.
Wapo wanaofanya hivyo kwa ajili ya kuenzi tamaduni zao, lakini pili ni kwa sababu ya kutaka kuyahifadhi mabaki ya miili hiyo kwa ajili ya kumbukumbu za kihistoria.
Hivi karibuni katika Mtaa Okaseni, Kata ya Uru wilayani Moshi kaburi la aliyewahi kuwa Mangi wa Wachaga wa Uru, Sabas Mushi lilifukuliwa na wazee wa ukoo na mabaki yake yalihifadhiwa sehemu maalumu.
Utaratibu wa ufukuaji wa mabaki ya mwili hufanywa na mmoja wa wazee wa heshima kwenye ukoo mwenye umri mkubwa, ambaye huhakikisha hakuna mabaki yanayosalia kaburini.
Inaelezwa kuwa ikibainika kuna mabaki ya mwili yaliyosalia kaburini kazi hiyo hurudiwa tena kwa madai kuwa yakibaki yanaweza kusababisha matatizo kwenye ukoo husika.
Baada ya kufukua masalia hayo, huchinja dume la ng’ombe kwa ajili ya kufanya sherehe tena kama ilivyofanyika wakati wa msiba wa mangi ambapo watu hula na kunywa vyakula vya aina mbalimbali.
Miongoni mwa makaburi ya mangi yaliyofukuliwa hivi karibuni ni pamoja na la aliyekuwa Mangi wa Wauru, Sabas; Mangi Kisarika Rindi na Mangi Laiseri Mushi.
Mmoja wa watoto wa Mangi Sabas, Raphael alipozungumza na Mwananchi alisema Wachaga wa Uru hufanya kitendo hicho kama ishara ya kuwaheshimu viongozi wao na kukumbuka yale waliyoyafanya enzi za uhai wao.
“Baada ya kuhakikisha kila mfupa umechukuliwa (kaburini), ngozi ya ng’ombe aliyechinjwa ikiwa bado mbichi hufungiwa yale masalia kisha yanaombewa na wazee wa ukoo na baadaye hupelekwa sehemu maalumu yakiwa yameviringishwa kwenye ile ngozi na kuhifadhiwa sehemu ambayo imeandaliwa kama kaburi.”
“Lakini wapo wengine huhifadhi kwenye vyungu na sehemu ambayo ni tulivu.’
Raphael alisema eneo linalohifadhi mabaki hayo watoto huwa hawaruhusiwi kufika. Hata hivyo hakueleza kwa nini hawaruhusiwi.
Mmoja wa wakazi wa Uru, James Massawe alisema kufukua mabaki ya mwili wa marehemu kwa kabila la Wachaga ni jambo la kawaida na wengi hufanya hivyo kwa sababu ya mila na desturi, lakini wengine hufukua kutokana na uhaba wa ardhi.
Alisema zipo familia zingine hufanya hivyo kwa ajili ya matambiko kwa madai ya kuondoa mikosi na baadaye mabaki hayo huhifadiwa sehemu yanakofanyikia matambiko huku wengine wakihifadhi katika miti mikubwa au maeneo ya mipaka ya makazi.